Na Theodos Mgomba, Dodoma
SERIKALI imesema haitaunda tume maalumu kufuatilia mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA, uliotokea mapema mwaka huu jijini Arusha.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo juzi, alipochangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama.
Dk. Nchimbi alisema yeyote mwenye ushahidi wa tukio hilo anapaswa kutoa taarifa ya ushahidi kwenye vyombo vya dola vinavyoshughulikia suala hilo, badala ya kutembea na ushahidi huo mifukoni au kwenye mikoba.
“Hakuna tume itakayoundwa kuhusu tukio la kurushwa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA. Yeyote mwenye ushahidi wa tukio hilo aupeleke kwa vyombo vya dola vinavyoshughulikia suala hilo,’’ alisema.
Waziri alisema kuna baadhi ya watu wanadai wana ushahidi wa nani aliyerusha bomu hilo lakini hawako tayari kuutoa kwa vyombo vya dola wakisubiri kuundwa tume huru itakayoshughulikia suala hilo.
“Kama suala ni kusubiri tume ili mtu akatoe ushahidi, hakuna tume itakayoundwa. Tumemshauri rais aunde divisheni ya makosa ya jinai ili kushughulikia masuala kama haya na yeye amekubali,’’ alisema.
Alisema kumekuwa na tabia ya watu kujichukulia sheria mikononi na kudhuru wengine, ikiwemo kufanya mauaji.
Dk. Nchimbi alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2007 hadi hivi sasa watu waliouawa kwa tabia ya kujichukulia sheria mikononi kwa kivuli cha wananchi wenye hasira wanafikia 4,055.
“Hii ni tabia mbaya na waache mara moja, serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wananchi wenye tabia hiyo,” alisema.
Akizungumzia suala la wafungwa, alisema kumekuwa na gharama kubwa ya kuwalisha walioko gerezani.
Waziri alisema hivi sasa zaidi ya sh. bilioni 25 hutumika kulisha wafungwa waliopo gerezani.
Tuesday, 17 December 2013
Dk. Nchimbi azima harakati za Lema
07:58
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru