Wednesday, 11 December 2013

Mawakili wa Ponda matatani


Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imeagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mawakili wa Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda.
Pia imetupilia mbali maombi ya marejeo ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro dhidi ya Sheikh Ponda kutokana na kuwepo dosari za kisheria katika hati ya kiapo.
Jaji Rose Teemba, akitoa uamuzi jana, ameagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mawakili wa Sheikh Ponda baada ya kubaini kufanyika udanganyifu katika hati hiyo.
Uamuzi huo aliutoa baada ya kusikiliza pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kupinga maombi hayo akidai hati ya kiapo ina kasoro za kisheria ambazo hazirekebishiki.
“Mahakama inatupilia mbali maombi ya kufanya marejeo kutokana na dosari zilizojitokeza katika hati ya kiapo iliyokuwa inayaunga mkono maombi.
“Nakubaliana na hoja za upande wa Jamhuri, kwa kuwa kabla ya pingamizi la awali niliziona dosari lakini nilikuja kushangaa kuona namna zilivyorekebishwa,” alisema Jaji Rose.
Ameagiza mawakili wa Sheikh Ponda wachukuliwe hatua za kinidhamu na vyombo vinavyohusika na masuala ya nidhamu kwa mawakili, kwa kuingilia nyaraka za mahakama.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, wakili Juma Nassoro, anayemtetea Sheikh Ponda alidai angewasilisha maombi mapya ya marejeo jana.
Sheikh Ponda kupitia mawakili wake aliwasilisha maombi hayo akiiomba mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Morogoro, uliokataa kumfutia shitaka la kukiuka amri halali ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, DPP aliwasilisha pingamizi la awali akipinga maombi hayo akidai ni batili, kwa kuwa hati ya kiapo kinachounga mkono kina upungufu, hivyo ni kinyume cha kifungu cha nane cha Sheria ya Viapo.
Wakati wa kusikiliza pingamizi hilo la awali, DPP aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, ambaye alitaja upungufu huo ni kutokuwepo tarehe katika  kiapo hicho, ambacho mwapaji ni wakili Hamidu Ubaidi.
Alidai kiapo hakijaeleza kama aliyeapa alifanya hivyo mbele ya wakili anayemfahamu na kwamba, kasoro hizo haziwezi kurekebishwa.
“Kutokana na kasoro hizo, naiomba mahakama ione ombi hili ni batili na halijawasilishwa kwa mujibu wa sheria,” alidai.
Akijibu hoja hizo, wakili Nassoro aliiomba mahakama itupilie mbali pingamizi hilo kwa sababu halina msingi kisheria, kwani ni maelezo.
Pia aliiomba mahakama iangalie ombi hilo kwa jicho la haki na si la kiufundi.
Nassoro alidai pingamizi hilo limewasilishwa kwa nia ya kuchelewesha kesi ili Sheikh Ponda aendelee kukaa rumande na shauri linalomkabili lisiendelee.
“Hakuna upungufu wowote katika kiapo hiki, kwani kinaonyesha kilichukuliwa Oktoba 8, mwaka huu, na ombi liliwasilishwa Oktoba 10. Kiapo kina tarehe na wakili aliyeapa alifanya hivyo mbele ya wakili anayemfahamu,” alidai.
Nassoro alidai inawezekana katika nakala za upande wa Jamhuri inaonekana kina upungufu lakini mahakama inaongozwa na nyaraka zilizo kwenye kumbukumbu za mashauri.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru