Wednesday 11 December 2013

CHADEMA yashitakiwa


NA KHADIJA MUSSA
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amekishitaki chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akitaka mwongozo kuhusu mgogoro unaokitafuna.
Mwigamba amemwomba msajili atoe mwongozo kutokana na kipengele cha ukomo wa madaraka ndani ya katiba ya chama hicho kubadilishwa.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, walivuliwa nyadhifa zao.
Mwigamba jana aliwasilisha malalamiko ofisi ya msajili akisema katiba ya CHADEMA ya mwaka 2004 kipengele 5.3.2 (C) inatamka kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena, ilimradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.
“Hata hivyo katiba ya chama ya mwaka 2006 kipengele cha 6.3.2 (C) inayozungumzia muda wa uongozi kimebadilishwa na sasa kiongozi aliyemaliza muda wake ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena ilimradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi,” alisema.
Alisema sentensi kuhusu ukomo wa uongozi haipo, kwani hata katika marekebisho ya katiba yaliyofanyika mwaka 2006 hayakuwa na mjadala wa kipengele kilichojadili kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi.
“Si kweli kwamba CHADEMA haijawahi kuwa na katiba ambayo ina ukomo wa uongozi, pia si kweli kwamba mwaka 2006 katiba mpya iliandikwa upya bali marekebisho yalifanywa kwa baadhi ya vipengele na kipengele kilichohusu ukomo wa uongozi hakikujadiliwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwigamba, anatumaini msajili atatoa mwongozo ili suala hilo lipatiwe suluhisho la kudumu ndani ya chama hicho.
Katika hatua nyingine, akizungumza na waandishi wa habari juzi, Albert Msando, ambaye ni mwanasheria wa Zitto, alisema mbunge huyo amewasilisha utetezi kwa mujibu wa katiba na kanuni za uendeshaji za chama hicho, baada ya kupokea barua yenye mashitaka 11 Desemba mosi, mwaka huu, iliyomtaka ajitete kwa maandishi.
Msando alisema licha ya kuwasilisha utetezi, Zitto ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, akieleza nia ya kukata rufani Baraza Kuu la chama hicho, kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake.
Alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za uendeshaji, alitakiwa kabla ya kuchukuliwa hatua angepewa mashitaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi jambo ambalo halikufanyika.
Msando alisema Zitto hahusiki na vurugu zozote zinazoendelea ndani ya chama hicho, pia aliwaomba wanachama kuwa watulivu, wavumilivu na waendelee kuwaheshimu viongozi wao wa kitaifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru