NA SAMASON CHACHA,TARIME
WENYEVITI wa vijiji vitano na wazee wa kimila wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya taifa ya Serengeti, mkoani Mara, wamesusia semina ya ujirani mwema na mahusiano, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Imeelezwa pia walisusia posho ya sh. 20,000, badala ya sh. 80,000 waliyoahidiwa kabla ya kuanza kwa semina hiyo ya siku sita.
Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kususia semina hiyo na kutoka nje ya ukumbi jana, wilayani Tarime, walisema poso hiyo ni ndogo hailingani na matumizi kwa kuwa wametoka vijiji vya mbali na wanajitegemea kwa kila kitu.
“Meneja wa Mawasiliano wa TANAPA, Pascal Shelutete akishirikiana na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mara, Emanuel Bwimbo, anayedaiwa si mwandishi wa habari ni mwalimu wa shule ya msingi Musoma, wamedai tusilipwe posho kama awali, badala yake tutalipwa sh. 20,000,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangucha, Patrick Sereka.
Wazee hao kwa pamoja, walisema kitendo hicho kiliwalazimu kususia semina hiyo na kudai kuwa uongozi wa TANAPA hauwajali viongozi wa vijiji na wazee wa kimila wanaozunguka hifadhi.
Walishutumu kwamba hali hiyo si ya kuleta mahusiano mema badala yake wanazidisha uhasama.
Katika semina hiyo, waandishi wa habari nao walizuiwa.
Hata hivyo, baadhi ya waandishi waliishutumu klabu yao kwa kuendekeza makundi ambayo yanawagawa.
Walisema hali hiyo ikiachwa iendelee itawaathiri.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru