Tuesday 3 December 2013

Nyaraka za ununuzi magari zaghushiwa


WIZARA ya Fedha imesema nyaraka nyingi za ununuzi wa magari si halisi, na hivyo serikali imeamua kutumia utaratibu wa kutambua bei halisi za magari katika kumtoza kodi mnunuzi wa gari husika.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), aliyetaka kujua Mamlaka ya Mapato (TRA) inatumia utaratibu gani katika kutoza kodi za magari.
Janet alisema serikali imegundua kuwa baadhi ya walipakodi wanatumia vibaya fursa ya kutozwa ushuru wa magari kwa kuangalia bei ya gari iliyoidhinishwa na nyaraka za ununuzi.
Alisema baadhi ya nyaraka za ununuzi si halisia kwani wanunuzi wa magari wanakuwa na makubaliano na wauzaji wa magari hayo ili ziweze kumsaidia mnunuzi kulipa kodi ndogo zaidi.
Naibu waziri alisema baada ya kugundua hivyo serikali imeamua kutumia
bei halisi ya gari katika kutoza kodi badala ya nyaraka hizo.
Alisema kazi hiyo hufanywa na TRA kwa kushirikiana na mawakala wa
kampuni za kutengeneza magari kama  Toyota (T) Ltd, na CMC katika kupata bei halisi ya magari mbalimbali katika masoko tofauti ya magari duniani.
Janet alisema bei hizo huchambuliwa na kuingizwa katika orodha ya serikali ya bei za magari na kutumika kuthamini na kukadiria  bei stahiki ya magari yanayoingia  nchini ambapo hutumika kama msingi wa kutoza ushuru wa magari.
Hata hivyo, waziri alisema bei elekezi inayowekwa kwa magari yaagizwayo nje ya nchi haipangwi kwa kuangalia mwaka lilipotengenezwa tu.
Pamoja na kuangalia mwaka gari lilipotengenezwa  na bei yake
kwa mwaka huo, pia huangaliwa muundo wa gari, mtengenezaji na ukubwa wa injini, alisema.
Hivyo alisema utaratibu wa sasa katika kutoza kodi za magari si kitendo cha dhuluma bali ni utaratibu unaozingatia vigezo vingi ambavyo pia hufuatwa na nchi nyingine duniani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru