Wednesday 18 December 2013

Dk. Sheni atoa maagizo mazito


Na mwandishi wetu, zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amemtaka Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha, kuhakikisha tanki la maji la Makunduchi linajengwa ndani ya miezi sita.

Agizo linalenga kumaliza tatizo la maji linaloukabili mji huo na maeneo mengine yanayouzunguka.
Dk. Sheni alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizindua Kituo cha Afya cha Kajengwa Makunduchi, mkoa wa Kusini Unguja.
Katika uzinduzi huo, wakazi wa Kajengwa walielezea tatizo la ukosefu wa maji katika eneo hilo linavyoathiri shughuli zao.
Dk. Sheni, alisisitiza kama tatizo ni fedha, wizara hizo zikae na kuangalia mafungu yatakayosaidia kupatikana kwa fedha hizo ili tanki hilo liweze kujengwa mara moja.
Pia, alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Mwalimu Haroun Ali Suleiman kwa kukiwezesha kituo cha afya Kajengwa kupata maji.
Waziri huyo amefadhili uchimbaji wa kisima hicho kwa gharama ya sh. milioni tano.
Aliwataka wakazi wa Kajengwa kuwa na subira wakati Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha huduma ya maji.
Alisema hatua hizo zimekuwa zikiungwa mkono na washirika mbalimbali wa maendeleo na alitolea mfano msaada wa visima 50 kutoka Serikali ya Ras Al Khaimah.
Rais Dk. Sheni, alisema baadhi ya maombi likiwemo la maji, walishamueleza katika ziara zake alizozifanya katika maeneo hayo.
Hivyo, alitumia fursa kwa Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati pamoja na watendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na Shirika la Umeme Zanzibar  (ZECO) kutoa maelezo kuhusu tatizo hilo.
Akitoa maelezo katika mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Ramadhani Abdalla Shaaban, alisema serikali inaendelea kutekeleza mpango wake wa kuongeza huduma za maji Unguja na Pemba.
Alisema wanatarajia ifikapo Septemba, 2014 tatizo hilo litakuwa limekwisha.
Shaaban, alisema katika eneo la Kajengwa Makunduchi, ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na kero kubwa ya maji kutokana na pampu ya kusukumia maji kuharibika.
Alisema kwa sasa tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi baada ya kufungwa pampu mpya.
“Lakini8 bado kuna kero, kwa kuwa kisima kilichopo hapa maji yake hayatoshelezi mahitaji,” alisema.
Akifafanua, Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dk. Mustafa Ali Garu, alisema tatizo la maji Kajengwa limeongezeka kufuatia kuharibika kwa tanki la maji lililoko Makunduchi Uwandani.
Alisema tanki hilo lilikuwa likisaidia kusambaza maji kijijini hapo.
Uzinduzi wa kituo cha afya Kajengwa ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kusirikiana na wadau wengine na Serikali, ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru