Tuesday, 3 December 2013

Ruzuku za walemavu zikaguliwe-Kikwete


KHADIJA MUSSA NA JOHN JOE (DACICO)
RAIS Jakaya Kikwete ameagiza fedha za ruzuku zinazotolewa kila mwaka kwa ajili ya kujengea uwezo vyama vya wenye ulemavu zifanyiwe ukaguzi unaostahili.
Pia ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri wa abiria vinaweka miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Rais aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani, ambayo kitaifa yalifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo aliahidi kuongeza ruzuku kwa vyama vya walemavu.
Alisema ni lazima wahusika kuzingatia kanuni za matumizi ya fedha ili kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete kila mwaka serikali inatoa ruzuku kwa ajili ya vyama vya watu wenye ulemavu na kuwataka wazingatie matumizi sahihi ya fedha hizo.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu, alisema serikali itahakikisha wanapata haki sawa bila kubaguliwa kwani hawana upungufu wa haki, wanastahili wapate kama binadamu wengine.
Alisema masuala ya haki na mahitaji kwa watu wenye ulemavu yataendelea kupewa kipaumbele cha juu na serikali kwa kuwa nao wana haki sawa ya kupata mahitaji ya msingi bila kubaguliwa.
ìMasuala ya haki na mahitaji muhimu yataendelea kupewa kipaumbele cha juu na yametungiwa sheria na shabaha ni kuweka muongozo wa kisheria, kisera juu ya namna ya kutoa huduma kwani kila mwananchi ana haki sawa ya kupata mahitaji ya msingi na kuwezeshwa bila kubaguliwa,î alisema.
Akizungumzia changamoto ya miundombinu ya usafiri, Rais Kikwete aliiagiza SUMATRA kuhakikisha wahusika wanasimamia kanuni bila kuoneana na kuweka miundombinu katika vyombo vya usafiri ili kuwawezesha walemavu kupata huduma hiyo bila ya usumbufu.
Alisema majengo mengi ya serikali yanayojengwa yamezingatia kuwepo kwa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, hivyo vyombo vya usafiri navyo vinapaswa kuzingatia hilo.
Kuhusu kutokuwepo kwa wakalimani katika vituo vya televisheni nchini, Rais Kikwete, alisema utekelezaji wa suala hilo umefika mbali licha ya kukabiliwa na changamoto ya wataalamu wa lugha za alama kudai ujira mkubwa.
Hata hivyo, alisema kutokana na umuhimu wa suala hilo wataliwezesha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kuanza kutumia wakalimali ili kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kupata taarifa mbalimbali.
Sambamba na hilo, Rais Kikwete, alisema serikali itaongeza fursa za elimu kwa kufufua vyuo vilivyopo na kujenga vipya pamoja na kutoa kipaumbele cha ajira kwa watu wenye ulemavu ili waweze kupata kazi na kujikwamua kiuchumi na hivyo kuondokana na utegemezi.
ìWalemavu wakiwezeshwa wanaweza hivyo tuna wajibu wa kuwawezesha na jamii inatakiwa iwatazame katika mtazamo chanya na nitaendelea kuwa bega kwa bega na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha haki zao,î alisema.
Aliwataka watu wenye ulemavu wanaopata vikwazo sehemu mbalimbali wanazokwenda kuomba ajira watoe taarifa ili waweze kusaidiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema mara nyingi ulemavu unatokana na matatizo ya kiafya, umasikini, mazingira duni pamoja na mila na desturi za jamii husika ambapo serikali kupitia wizara ya afya inawahudumia watu hao kwa kuondoa vizuizi vinavyowakabili ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kuhusu kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ambayo ni ëOndosheni vizuizi, fungueni milango kwa ajili ya jamii jumuishi kwa woteí, alisema ndio dira na kichocheo muhimu cha kuhamasisha wanachi na serikali kufahamu na kutekeleza masuala ya watu wenye ulemavu.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Amon Anastazi alimshukuru Rais Kikwete kutokana na serikali kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu wenye ulemavu na kwamba historia itaandika.
ìSerikali yako imewesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye ulemavu kupata elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu pamoja na kupitisha sheria namba tisa ya haki ya watu wenye ulemavu,î alisema.
Hata hivyo, Anastazi kwa niaba ya watu wenye ulemavu, aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hususan idara ya ustawi wa jamii kwa kuhusika moja kwa moja katika kusimamia haki, mahitaji na huduma za kiutengamano kwao kwa kutoa ruzuku kwa vyama vyote 10 vinavyounda SHIVYAWATA katika kusaidia gharama muhimu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru