Tuesday 3 December 2013

CHADEMA basi


Waandishi Wetu,Singida na Arusha
MZIMU wa kuvuliwa uongozi ndani ya CHADEMA, Zitto Kabwe na wenzake, umeendelea kukitafuna chama hicho na kukiacha vipande vipande, baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu, kutangaza kujiuzulu.
Kitundu amesema hawezi kuendelea kuwa kiongozi katika chama hicho, wakati viongozi wa ngazi za juu hawakubali mawazo mbadala na amemtaka Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe naye ajiuzuru kwa kuwa ameshindwa kazi.
Alitamka kujiuzulu jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Singida na kumtaka Mbowe kuivunja Kamati Kuu kwa kuwa imeshindwa kukiuganisha chama hicho na aueleze umma na wanachama katika mikoa yote sababu za kumvua uongozi Zitto.
Kitundu alisema licha ya kujiuzuru Uenyekiti chama hicho, atapambana hadi tone la mwisho la damu yake kuhakikisha demokrasia ya ndani ya CHADEMA inaheshimiwa na kwamba Watanzania hawadanganywi tena.
Alisema kamati kuu imekurupuka na kufanya uamuzi uliotawaliwa na hofu, chuki na uroho wa madaraka dhidi ya Zitto na wenzake walioonyesha nia thabiti ya kukivusha chama kwenye harakati za kulikomboa taifa.
Kitundu alisema kitendo cha kamati kuu kuwavua uongozi ni sawa na mtu kuanza kujenga nyumba ya matofali mabichi wakati
wa masika mvua nyingi zinanyesha na kwamba nyumba hiyo haitakuwa salama.
Alisema CHADEMA kilikuwa na kila dalili ya kushika dola na kwa njia hiyo, kingewakomboa Watanzania na wao waasisi wangenufaika lakini kwa sasa kimeghubikwa na mfumo wa kudidimiza siasa katika chama.
“Tunapenda wanachadema na Watanzania, watambue kuwa hatuna imani na Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Willibod Slaa na kamati kuu kwa ujumla na tunaagiza Mwenyekiti aivunje mara moja na yeye ajiuzulu,” alisema.
Mbali na hilo, Kitundu amemuonya Dk.Slaa kukanyanga mkoani humo, ikiwa bado hajayafanyia kazi maelekezo ya CHADEMA mkoa wa Singida.
Tangu avuliwe uongozi Zitto, mjumbe wa Kamati Kuu, Dk.Kittila Mkumbo na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, chama hicho kimekumbwa na janga la viongozi kujiuzuru.
Viongozi hao ni Makamu Mwenyekiti Bara, Said Arfi, Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi ambao wote wanapinga hatua ya kuvuliwa uongozi Zitto kwa kuwa imekwenda kinyume na taratibu na ni uonevu.
Ofisi zachomwa moto Arusha
OFISI ya wilaya na mkoa wa CHADEMA mkoani Arusha, zimechomwa moto na watu wasiojukana katika kipindi ambacho sintofahamu ndani ya CHADEMA imetawala tangu Zitto na wenzake  kung’olea madarakani.
Akizungumza na Uhuru, Diwani wa CHADEMA   Kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro, alisema ofisi hizo zilichomwa moto jana, eneo la Ngarenaro jijini hapa.
Nanyaro alisema ana wasiwasi ofisi hizo, zilichomwa moto saa moja asubuhi kwa kuwa hali hiyo ilionekana saa mbili asubuhi
baada ya ofisi hiyo kufunguliwa na kukuta  moto ukiwa bado haijazimika.
Alisema ofisi hizo ambazo ziko katika jengo moja ziliungua eneo la juu (dari), lakini hakuna madhara makubwa moto huo ulizimwa.
Nanyaro alisema ana wasiwasi tukio hilo limefanywa na watu aliowaita wahujumu wa chama chao wakiwemo waliofukuzwa hivi karibuni.
ìNi kweli ofisi imechomwa moto eneo la juu huenda mtu alikuja na kutupia moto juu ya paa lakini hawajafanikiwa malengo yao maana ni dari tu na mbao zilizoshikilia ndio zimeungua,î alisema Nanyaro.
Nanyaro alisema anahisi watu hao walikuwa na njama za kuchoma kompyuta zilizoko ili  kupoteza nyaraka muhimu ikiwemo orodha ya wanachama.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, aliyejitambulisha kwa jina moja la Lusingu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba maelezo zaidi yalikuwa yakitolewa ofisi ya polisi wilaya ya Arusha kwa ajili ya upelelezi wa awali.
Alisema polisi inawashikilia watu wawili ambao ni Jenipher Mwasha (22) ambaye ni katibu muhtasi wa CHADEMA na mlinzi Kitabuzi Bahati (42).
Alisema taarifa alizonazo watu hao walikuwa na lengo la kuteketeza ofisi tatu za CHADEMA zilizoko katika jengo hilo.
Lusingu alisema uchunguzi utakapokamilika watatoa taarifa kamili kuhusu tuko hilo kwa vyombo vya habari.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru