NA MWANDISHI WERU
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amewazodoa wanaotafuta madaraka kuwa uongozi hautafutwi kwa udi na uvumba wala kwa rushwa bali anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii.
“Anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii husika kutokana na ubora wake na siyo vishawishi vyake. Ni ukweli uliowazi kuwa uchaguzi wetu sasa umegubikwa na rushwa na vishawishi vingi na siyo ubora, uhodari wala tabia ya anayetaka nafasi hiyo ya uongozi,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa: “Hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za kuwanunua wapiga kura vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi ngazi ya urais. Huu ni utaratibu wa hatari na lazima tuupige vita kwa pamoja.”
Sumaye aliyasema hayo jana wakati wa kuchangia ujenzi wa ukumbi wa Parokia ya Mawella ya Kanisa Katoliki jimbo la Moshi.
Alisema wakati Watanzania wanasubiri kuingia mwaka mpya wa 2014, wanapaswa kutambua kuwa huo ni mwaka muhimu kwa kwa mustakabali wa taifa kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi katika ngazi za serikali za mitaa na ni mwaka wa maandalizi kwa uchaguzi mkuu.
“Nataka niliweke wazi tangu mwanzo kuwa mimi siisemi serikali yangu wala sitamsema mtu yeyote bali nitakayoyasema na siyo mara yangu ya kwanza kuyasemea ni kupiga vita tabia mbaya. Katika kukemea mabaya hayo inawezekana mtu akajihisi anasemwa kama hayo mabaya anayafanya. Dawa siyo kumchukia anayekemea tabia hiyo mbaya, bali ni kuachana nayo,” alisema.
Aliendelea kufafanua kuwa katika utaratibu wa demokrasia sahihi na halisi wapiga kura hutakiwa kuwachagua viongozi au kiongozi kufuatana na sifa nzuri za uongozi alizonazo mgombea kama vile ushupavu, uaminifu, uadilifu na nyingine muhimu.
Sumaye alisema kama ilivyokuwa zamani, mtu anayetakiwa kuwa kiongozi anatafutwa na jamii na siyo yeye kusaka uongozi.
“Mbaya zaidi ni pale msaka uongozi atakapotafuta nafasi hiyo kwa njia zisizofaa kama vile rushwa na kuwanunua wapiga kura....utaratibu wa kuwekwa au kuchaguliwa katika nafasi bila vishawishi vya rushwa uliotumika tangu enzi za kale ndiyo unaotakiwa kutumika hadi sasa, labda kwa kuboreshwa kutegemeana na mazingira,” alisema.
Huku akinukuu baadhi ya vifungu katika Biblia, alisema wananchi wanapaswa kuigopa rushwa kwa kuwa hata vitabu vya dini vimeikemea.
Alisema kiongozi mtoa rushwa hafai kuchaguliwa kwa kuwa hawezi kuwafikisha mahali popote wananchi na badala yake atatumia nafasi atakayopewa kutengeneza maslahi yake binafsi na marafiki zake.
Sumaye alisisitiza kuwa: “Huo ndiyo mwisho wa upeo wa macho yake kuona. Ataona ndani ya duara lake na marafiki zake na wengine akitutazama anaona giza tu kwa sababu kwetu, yeye amepofuka na tuko nje ya duara la upeo wa macho yake.”
Kutokana na hali hiyo aliwaomba viongozi wa dini kushiriki kikamilifu kupiga vita vitendo viovu vya rushwa, ufisadi, kuuza dawa za kulevya au kuua.
Alisema wakati wa kuingia kwenye kipindi cha uchaguzi, hivi sasa kuna mambo yameanza kujitokeza ikiwemo fadhila kuwa nyingi kwa baadhi ya wanaowania nafasi hasa zile za juu.
“Fadhila zimeanza kuwa nyingi katika baadhi ya sehemu na kwa baadhi ya nafasi hasa nafasi za juu na wapiga kura tayari wameanza kupigwa mnada na kupangiwa bei kulingana na uhodari au umuhimu wa nafasi aliyonayo mhusika. Haya ni mambo machafu ambayo hatutakiwi tuyafumbie macho bali tupambana nayo kwa nguvu zote,” alionya Sumaye.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi anazofanya kupambana na uoza wa rushwa katika jamii, hasa rushwa nyakati za uchaguzi.
Pia, Sumaye alibainisha kuwa hatakoma kupiga vita rushwa na kuwa anafanya hivyo sio kwa malengo ya kuwania urais mwaka 2015, bali anatimiza wajibu kwa nchi yake.
Saturday, 28 December 2013
Sumaye awazodoa wasaka madaraka
07:39
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru