Saturday, 21 December 2013

CCM imepata pigo- Mwigulu


NA TUMAINI MSOWOYA, MBARALI
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, ameongoza mamia ya wakazi wa mikoa ya Iringa na Mbeya katika mazishi ya aliyekuwa Katibu wa CCM mkoani Iringa, Emmanuel Mteming’ombe yaliyofanyika kwenye makaburi ya Rujewa Mkoa wa Mbeya.

Akitoa salamu za mwisho katika mazishi hayo, Mwigulu ambaye muda mwingi alikuwa akibubujikwa na machozi, alisema kitu pekee kitakachowaunganisha wanachama wa CCM ni upendo wa kweli, hasa wakati wa furaha, huzuni na misiba.
Nchemba alisema Chama kimepata pigo kwa kuondokewa na kiongozi ambaye alitegemewa katika kuendelea kukijenga.
Alisema upendo wa kweli haubagui, bali unajali utu na kwamba, baada ya msiba huo lazima uonekane kwa familia ya kiongozi huyo akiwemo mkewe na watoto.
“Lazima kuwe na upendo wa dhati miongoni mwetu ili tuendelee kuwa na umoja na mshikamano wa dhati, Mteming’ombe ameondoka wakati CCM inamhitaji na mchango wake katika kuijenga CCM yetu tuuenzi kwa kuipenda familia yake,”alisema Mwigulu ambaye muda mwingi alibubujikwa na machozi.
Aliwataka viongozi wa serikali na Chama hicho kujenga tabia ya kufanya kazi karibu na watu na sio kujibagua kwa kujiona bora kuliko jamii waliyoamua kuitumikia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema mkoa huo umesikitishwa kuondokewa na kada waliyemuamini ambaye aliweza kufanya kazi kwa uadilifu katika mikoa mingine na kwamba, aliendelea kuwa mshauri wa karibu kwa CCM katika mkoa.
“Alikuwa Iringa lakini alikuwa mshauri wetu wa karibu. Tumeumia sana kumpoteza kada wetu ambaye tulimhitaji,”alisema Kandoro.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, alisema mkoa wa Iringa umepata pengo ambalo halitaweza kuzibika kwa madai kuwa kifo cha Mteming’ombe kimetokea wakati ambao hakuna aliyetarajia.
“Niliwahi kufanya kazi na Mteming’ombe nikiwa mkoani Ruvuma na baadaye Iringa, imeniumiza sana lakini sina ujanja kwani namuachia Mungu ambaye ndiye aliyeruhusu haya yatokee,”alisema Dk. Christine.
Mkuu huyo alisema, alibahatika kumjulia hali wakati alipougua, lakini haikuonyesha kama hali yake ingeweza kusababisha mauti kama ilivyotokea.
Akisoma wasifu wa marehemu huyo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema kiongozi huyo alifariki siku moja baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa akisumbuliwa na homa ya matumbo pamoja na athma.
Hata hivyo alisema, wiki mbili kabla ya kufariki alianza kuumwa na kwamba alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani hadi siku alipozidiwa.
Kabla ya kuwa Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Mteming’ombe alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Mbeya, Diwani wa Kata ya Rujewa Wilayani Mbarali, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Rujewa na Katibu wa CCM wa wilaya za Kyela, Ileje na Mbozi.
Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Katibu wa CCM mkoani Mbeya, Ruvuma na hatimaye Iringa ambako mauti yamemkuta. Mteming’ombe ameacha watoto watatu na mjane.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru