Sunday 7 July 2013

Abiria toeni taarifa -SUMATRA


NA MWANDISHI WETU, KIBAHA
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchini Kavu (SUMATRA), imewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, hususan wanaokatisha safari.
Imesema katika kukabiliana na madereva hao, watashirikiana na Jeshi la Polisi. Pia itawadhibiti wanaokusanya nauli bila kutoa tiketi kwa abiria.
Ofisa Mwandamizi wa SUMATRA mkoa wa Pwani, Iroga Nashoni, alisema hayo mwishoni mwa wiki, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema abiria wanapaswa kushirikiana na chombo hicho kama baadhi yao wanavyotoa taarifa polisi ili kuondoa kero kwa wasafiri.
Nashoni alisema mamlaka  imefungua ofisi mkoani Pwani ili kusogeza huduma kwa wateja.
Alisema ofisi zingine zitafunguliwa Singida, Iringa, Musoma na Rukwa, ili kupanua wigo na kuongeza ufanisi wa kazi.
Ofisa huyo alisema changamoto kubwa mkoani hapa ni mabasi, hususan ya Mlandizi na Kongowe kushindwa kumalizia safari (kukatisha ruti) kama inavyojieleza katika ratiba ya safari (TLB).
Alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kujua haki ya kutoa taarifa katika idara hiyo.
SUMATRA pia inafanya  operesheni za kushitukiza ili kukamata magari yanayokiuka sheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru