Sunday 7 July 2013

Wazee wataka serikali mbili


NA YASSIN KAYOMBO, KIGOMA
BARAZA la Wazee wa CCM wilaya ya Kigoma Mjini, limependekeza kuendelea muundo wa serikali mbili, badala ya tatu ulipoendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pendekezo hilo walilitoa mwishoni mwa wiki mjini hapa, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, Mabaraza ya Jumuia ya Wazazi, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani humo.
Kikao hicho kilihutubiwa na  Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, aliyekuwa ziarani kukagua na kuhimiza uhai wa Chama na jumuia zake na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Akisoma tamko kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa baraza hilo, Abdul Singiso, alisema Muungano wa serikali mbili hauna budi kuendelea kuwapo, kwani ndiyo ulioleta mshikamano wa kitaifa.
Singiso alisema mapendekezo yaliyotolewa katika rasimu ya katiba mpya ya kuwa na serikali tatu hayana tija kwa taifa.
“Wazee wa Kigoma Mjini tunadhani Muungano wa serikali tatu ni mwanzo wa kuvunja amani, umoja na mshikamano uliopo. Una mwelekeo wa kuuvunja Muungano uliodumu kwa miaka mingi,” alisema.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika rasimu ya kwanza iliyotolewa imependekeza muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa wazee hao, muundo huo pia utaongeza mzigo kwa walipakodi, kwa kuwa watalazimika kulipa zaidi kwa ajili ya uendeshaji wa serikali hizo.
Ili kuimarishXa mshikamano, upendo na umoja wa kitaifa, walipendekeza Watanzania waanze kufikiria kuwa na muundo wa Muungano wa serikali moja utakaowapunguza mzigo wa uendeshaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru