Friday 5 July 2013

Katibu Mkuu Kiongozi afagilia magazeti ya Uhuru, Mzalendo


NA KHADIJA MUSSA

KATIBU  Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameipongeza Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, kuwa ni mfano wa kigezo cha uandishi bora wa habari unaofuata maadili.
Alisema mara zote yamekuwa yakiandika habari bila kuupotosha umma.
Pongezi hizo pia alizitoa kwa magazeti ya Serikali ya Habari Leo na Dailynews, kuwa yako mstari wa mbele katika kuchapisha habari kwa kufuata maadili ya taaluma.
Aliyasema hayo jana alipotembelea banda la Kampuni ya Tanzania Standard Newspaper (TSN), katika Viwanja vya Maonyesho ya 37 ya Kimataifa ya Biashara, yanayoendelea  katika viwanja vya maonyesho vya Mwalimu J.K. Nyerere, maarufu kama Sabasaba.
Alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma.
Balozi Sefue, alisema kuna baadhi huamua kuupotosha umma kwa makusudi, bila kujali athari zitakazoweza kujitokeza.
“Tabia hii, huwezi kuikuta katika magazeti ya Uhuru, Mzalendo wala Habari Leo na Daily News,” alisema Katibu Mkuu huyo Kiongozi.
Alivitaka vyombo vingine kujifunza toka kwa magazeti hayo ya Chama na Serikali.
Alisema kwa sasa kuna vyombo vya habari vinavyofanya kazi kinyume cha maadili kwa kutoa habari ambazo siyo sahihi kwa madai ya kufanya biashara.
Balozi Sefue, alisema biashara isiwe kigezo cha kuandika habari zisizo na ukweli zenye kulenga uchochezi.
Sefue, alitembelea katika mabanda tofauti ya maonyesho yakiwemo ya Baraza la Kiswahili Tanzania, Kampuni ya kuchapisha vitabu ya Mkuki na Nyota pamoja na banda la Radio Maria.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru