Sunday 7 July 2013

Usikilizaji rufani ya Muro wasimamishwa


NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesimamisha usikilizwaji wa rufani iliyokatwa na upande wa Jamhuri, kupinga kuachiwa huru aliyekuwa mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake.
Hatua hiyo inatokana na upande wa Jamhuri kuwasilisha taarifa ya kukata rufani, Mahakama ya Rufani Tanzania, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali moja ya sababu za kupinga uamuzi wa kuachiwa huru Muro na wenzake, uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu, aliitupilia mbali sababu ya Jamhuri kutaka kesi ya kuomba na kupokea rushwa iliyokuwa inawakabili Muro, Edmund Kapama na Deogratius Mgasa, irudishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili ikasikilizwe upya.
Uamuzi wa kusimamisha mwenendo wa rufani ulitolewa wiki iliyopita na Jaji Dk. Fauz, baada ya upande wa Jamhuri kuomba hivyo ili kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani.
Juni 3, mwaka huu, wakati rufani iliyokatwa na upande wa Jamhuri ilipotajwa kuendelea kusikilizwa kwa sababu zingine za rufani, Wakili wa Serikali Mwandamizi Lilian Itemba, aliomba usimamishwe hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi.
Alisema iwapo Mahakama Kuu itamalizia kusikiliza sababu zingine uamuzi wa Mahakama ya Rufani unaweza kuathiri  zilizobaki.
Muro na wenzake walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kuomba na kutaka kupokea rushwa ya sh. milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.
Waliachiwa huru na Hakimu Mkazi Frank Moshi wa Mahakama ya Kisutu, ambapo serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ilikata rufani Mahakama Kuu, kupinga kuachiwa huru kwa Muro, Mugasa na Kapama.
DPP anadai mwenendo mzima wa shauri hilo ulikuwa haueleweki, hivyo kusababisha hakimu kufikia uamuzi usio sahihi.
Kwa mujibu wa DPP, sababu zingine ni hakimu alikosea kuchambua ushahidi uliokuwa umetolewa, ambao ulisababisha kufikia uamuzi usio sahihi.
Pia anadai hakimu alikosea kuwaachia washitakiwa bila kuzingatia ushahidi uliotolewa mahakamani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru