Monday 8 July 2013

Wadau wa mafuta wapinga zabuni


NA MWANDISHI WETU
WADAU wa mafuta wamepinga zabuni ya Uagizaji Mafuta ya Akiba ya Taifa  (SPR) iliyoitishwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa madai kampuni zilizoongoza zimekiuka sheria na utaratibu.
Inadaiwa kuwa moja ya sababu za kupingwa kwa kampuni hizo mbili ni kutokana na kuwa na ushirikiano wa kibiashara, jambo ambalo halikubaliki kwa mujibu wa utaratibu wa zabuni hiyo.
Kampuni zinazopingwa ni Vitol ya Uswisi na Oman Trading International (OTI), ambazo
zimeshika nafasi ya kwanza na ya pili.
Inadaiwa kuwa kampuni hizo ziliingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kusaidiana kwenye biashara mbalimbali.
Ushirikiano huo umeonyeshwa wakati wa kusafirisha nje ya nchi bidhaa za Oman za Kampuni ya Salalah Methanol Company and Aromatics LLC, ambapo kampuni hizo zimeshirikiana.
Kampuni 25 zilijitokeza katika zabuni hiyo ya uagizaji mafuta ya akiba ya taifa, zikiwemo za Independent Petroleum Group ya Bahama, Galawa Petroleum Limited na Prevail Technologies Tanzania ya hapa nchini.
Nyingine ni Trafigura Pte, Addax Energy SA na Augusta SA Geneva, zote zenye makao
yake makuu Geneva, Uswisi.
TPDC ilitangaza zabuni ya kuagiza mafuta hayo ili kulinda soko la mafuta nchini, kutokana na kuchezewa na baadhi ya wafanyabiashara wanaotaka kujipatia faida maradufu.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha.
Sababu nyingine ya kutangaza zabuni hiyo ni kutokana na baadhi ya kampuni za mafuta kukataa kupunguza bei kwa kuyafanya yaonekane yameadimika, jambo lililozusha tafrani mwaka 2011.
Miongoni mwa masharti ya zabuni ya TPDC, ilikuwa kampuni husika kukubali kuuza mafuta kwa kampuni ya COPEC ambayo ni ya serikali, inayoendeshwa chini ya TPDC.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Yona Killaghane, alikaririwa na gazeti la Serikali jana, kuwa wanayafanyia uchunguzi madai hayo, ili kubaini kama kuna dosari zilizojitokeza.
Pia, alisema madai hayo ya wadau hayajawasilishwa rasmi TPDC, lakini hilo halitazuia kufanyika kwa uchunguzi.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru