Friday 5 July 2013

Kifua Kikuu chashika kasi


NA MOHAMMED ISSA
SERIKALI imesema ugonjwa wa kifua kikuu bado ni tatizo sugu.
Imesema utafiti unaonyesha ugonjwa huo unawapata zaidi wanaume kuliko wanawake na kwamba, wazee ndio waathirika wakubwa kuliko vijana.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipozindua taarifa ya utafiti wa kwanza wa kutathmini kiwango cha tatizo hilo nchini.
Alisema idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu inazidi kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ugonjwa wa ukimwi na makazi hafifu.
Dk. Mwinyi alisema wataendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema hadi sasa vituo 900 vimeshajengwa kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa tiba.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi alisema Tanzania imevuka lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa kutibu wagonjwa wa kifua kikuu, ambapo asilimia 85 ya wanaotibiwa wanapona.
Alisema licha ya kuvuka lengo, Tanzania imeanza kutoa matibabu kwa wagonjwa sugu wa ugonjwa huo.
Waziri alisema utafiti unaonyesha ugonjwa huo umeathiri zaidi wananchi wa Tanzania Bara kuliko Zanzibar.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Blasdus Njako, alisema utafiti unaonyesha wananchi wengi wa vijijini hawajitokezi kupima ugonjwa huo.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru