Tuesday 9 July 2013

Ofisa JKT kortini kwa meno ya tembo


NA FURAHA OMARY
OFISA Uvuvi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Selemani Chasama, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shitaka la kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni nne.
Chasama (50), mkazi wa Mbezi Makabe, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa shitaka mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba.
Mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili Braysoni Shayo, anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2013.
Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, alidai Julai 4, mwaka huu, eneo la Mbezi Makabe, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, mshitakiwa alikutwa na nyara za serikali.
Alidai mshitakiwa alikutwa na vipande 347 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya dola za Marekani 2,610,000 (sh. 4,249,080,000), mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kibali.
Hakimu Nyigulila alisema mshitakiwa hatakiwi kujibu chochote, kwa kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza, labda Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atoe kibali isikilizwe na mahakama hiyo.
Kimaro alidai upelelezi haujakamilika, hivyo kuomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Nyigulila aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, mwaka huu, ambapo mshitakiwa yuko chini ya ulinzi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru