Wednesday 17 July 2013

JK ampa kazi Rais wa Sudan


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amemtaka Rais Omar al Bashir wa Sudan, kuchukua hatua haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na mauaji ya askari saba wa Tanzania.
Askari hao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliuawa wakilinda amani katika jimbo la Darfur, nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Kikwete alisema hayo kupitia mazungumzo kwa simu na Rais Bashir.
Rais Kikwete ametaka wote waliohusika wafikishwe mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.
Katika mazungumzo yao, Rais Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kuahidi kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.
Rais Bashir alisema anaamini waliohusika ni wahalifu, hivyo ni lazima watasakwa na kuchukuliwa hatua.
Kiongozi huyo amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha, kwa kuwa wanajeshi wa Tanzania wako Sudan kulinda amani na usalama wa wananchi wa nchi hiyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alimpigia simu Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo uliotokea wakati askari hao wakitekeleza jukumu la kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi kilichokiri kuhusika na shambulio hilo, ingawa kumekuwa na kutupiana lawama kati ya vikundi vya kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano kati ya vikundi vya kikabila na koo yamesababisha uvunjifu wa amani na usalama katika jimbo hilo kwa miaka 10 sasa. Mapigano hayo yamesababisha vifo kwa wananchi wa Sudan na wageni.
Mwishoni mwa mwaka jana wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa jirani na El Geneina, Magharibi mwa Darfur.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi takriban 50 wameuawa tangu kikosi cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa pamoja chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze operesheni mwishoni mwa mwaka 2007.
Taarifa za UN zinaeleza kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania Jumamosi iliyopita, wanajeshi sita wanaolinda amani Darfur waliuawa tangu Oktoba mwaka jana, huku watu 300,000 wakiripotiwa kuyakimbia makazi yao.
Kiini cha mgogoro huo kinasadikiwa kuwa ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo.
Miili ya askari wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya maziko.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru