Tuesday 9 July 2013

TRL kukarabati vichwa vinane


Na Hamis Shimye
UONGOZI wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), umepanga kukamilisha ukarabati wa vichwa vinane vya treni katika mwaka huu wa fedha.
TRL pia imepanga kununua vichwa 13 vipya vya treni na mabehewa mapya 22 ya abiria, kununua mabehewa 274 ya mizigo, 25 ya kubebea kokoto na 34 ya breki.
Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Kipallo Kisamfu, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu  mipango ya kampuni hiyo kwa mwaka huu wa fedha.
Alisema kampuni imejipanga kikamilifu kuhakikisha inatoa huduma bora kwa umma, kwa kuwa reli ndiyo msingi wa uchumi wa taifa.
Kisamfu alisema katika bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014, TRL imetengewa sh. bilioni 137.6 ili kukamilisha miradi iliyokwisha kuanzwa.
Katika hatua nyingine, alisema usafiri wa treni jijini Dar es Salaam unarejea leo, baada ya kukamilika matengenezo ya kichwa cha treni mkoani Morogoro.
Alisema usafiri huo unarejea baada ya kusimama kwa siku mbili kutokana na kuharibika kwa kichwa kimoja kati ya vitatu vinavyotoa huduma hiyo.
Kisamfu alisema usafiri wa treni hiyo unaisababishia hasara serikali kutokana na uendeshaji kuwa wa gharama kubwa.
Alisema hasara hiyo inatokana na treni inayotumika kuwa ya masafa marefu.
Hata hivyo, alisema TRL ipo katika mchakato wa kununua treni kwa ajili ya usafiri huo, ambapo mazungumzo yanafanyika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru