Monday 8 July 2013

Cameron ampa tano Murray


NA MWANDISHI WETU
LONDON, England
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amesema kuwa mchezaji tenisi nguli, Andy Murray, alistahili kutwaa ubingwa wa michuano ya Wimbledon.
Caron, ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Murray, kutwaa taji hilo juzi usiku baada ya kumshinda mpinzani wake mchezaji namba moja kwa ubora wa tenisi duniani, Novak Djokovic.
Hii ni mara ya kwanza kwa raia wa Uingereza, kutwaa taji hilo baada ya miaka 77 tangu mwaka 1936 na Murray, alitwaa taji hilo kwa ushindi wa seti 6-4 7-5 6-4.
"Sidhani kama kulikuwa na mtu ambaye angetwaa taji hili zaidi ya Murray. Ni faraja kubwa kwa sababu tulisubiri kwa miaka mingi kutwaa taji la Wimbledon," alisema Cameron.
Waziri Mkuu huyo alisema Murray amekuwa shujaa wa Uingereza na kipaji chake cha mchezo wa tenisi ni cha hali ya juu.
Cameron, alisema kuwa muda mfupi kabla ya mchezo huo, Jumapili asubuhi maelfu ya raia wa Uingereza walikuwa na shauku kubwa ya kuona Murray akitwaa taji hilo.
Murray, alidokeza kuwa ana furaha kubwa kuipa Uingereza heshima ya kutwaa taji hilo na kuongeza kuwa alicheza kwa lengo la kuiletea sifa nchini yake.
Watu maarufu walimiminika kwenye uwanja huo kushuhudia mchezo huo akiwemo nguli wa Manchester United Wayne Rooney na mkewe, Coleen.
Pia, mke wa nahodha wa zamani wa England, David Beckham, Victoria 'Posh Spice' alikuwepo kumpa sapoti mchezaji huyo aliyeweka historia.
 Mchezaji huyo mwenye miaka 26, alifanyiwa tafrija kamambe ya kupongezwa kwa ushindi huo ambapo watu maarufu walihudhuria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru