Friday 19 July 2013

Tanzania kuuza gesi nje ya nchi


NA SELINA WILSON
SERIKALI inakusudia kujenga kiwanda cha gesi kwa ajili ya mauzo ya nje, ambapo kitaliwezesha taifa kuvuna mapato ya dola za Marekani milioni 200 (sh. bilioni 320) kwa mwaka.
Imesema kiwanda hicho kitajengwa eneo la Rushungi, ambalo liko katikati ya mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba, mchakato wa ujenzi wake unaendelea na kampuni mbili zimeonyesha nia ya kuwekeza.
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli wa Wizara ya Nishati na Madini Injinia Hoseah Mbise, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam.
Injinia Mbise, alikuwa akizungumza kuhusu faida zitokanazo na gesi asilia na manufaa yake kwa Watanzania, ikiwa ni utaratibu wa wizara mbalimbali kukutana na vyombo vya habari kueleza utekelezaji wa kazi za serikali.
Alisema mradi huo ni mkubwa na utekelezaji wake utachukua miaka mitano hadi sita na unatarajiwa kukamilika ifikiapo 2020.
Alisema kiwanda hicho kitakuwa kinachakata gesi asilia (LNG) na kuisafirisha kwa bomba kwa mauzo ya nje ya nchi.
Alizitaja kampuni zilizoonyesha nia ya kutekeleza mradi huo ambazo zinafanya mazungumzo na serikali kuwa ni BG ya Uingereza na State Oil ya nchini Norway.
Akizungumzia faida za gesi asilia, Injinia Mbise, alisema tangu 2004 hadi mwaka huu, sh. trilioni saba zimeokolewa kutokana na kutumia gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Alisema hadi Desemba 2012 sh. milioni 885 zimelipwa kwa Halmashauri ya Kilwa kama kodi ya huduma na kwa sasa, zaidi ya asilimia 50 ya umeme nchini unazalishwa kwa gesi asilia.
Tangu 2004 hadi sasa, megawati 418.5 za umeme zinazalishwa kutokana na gesi asilia.
Utafiti wa mafuta na gesi nchini ulianza 1952 hadi 1974, ambapo kampuni ya Agip ya Italia ilifanikiwa kupata gesi katika eneo la Songosongo na 1982 eneo la Mnazi Bay.
Hata hivyo, wataalamu wa kampuni hiyo waliondoka bila kuivuna gesi hiyo baada ya kuhisi kuwa kuna kiasi kidogo, baadae kampuni zingine zilifanya utafiti na kuanza kuvuna nishati hiyo.
Kwa sasa, kuna kampuni 19 na mikataba 27 ya utafutaji mafuta na gesi katika maeneo ya nchi kavu, mwamba na katika kina kirefu cha bahari.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru