Wednesday 3 July 2013

Maswi awatangazia kiama wala rushwa


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetangaza kiama kwa watumishi watakaojihusisha na rushwa, kuwa watatimuliwa kazi bila kujali madaraka yao.
Onyo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wakati akizungumza kwenye kongamano lililoandaliwa kwa ajili ya wadau kutoa maoni juu ya utekelezaji wa miradi 29 katika sekta ya nishati.
Miradi hiyo imo kwenye mpango wa serikali wa matokeo makubwa kwa muda mfupi, lililofanyika jana, mjini Dar es Salaam.
Alisema wananchi na wadau wanapaswa kutoa taarifa za kuombwa rushwa zilizosababisha kukwama kwa baadhi ya miradi ili hatua zichukuliwe mara moja.
Maswi, alisema wafanyakazi wa serikali hususan wizarani kwake, wanapaswa kuwa waadilifu.
“Kama mtaalam au kamishna atajaribu kula rushwa sitakuwa na msamaha wala kigugumizi katika kuchukua hatua, tumekubaliana kufanya kazi kwa uadilifu,” alisema.
Alidai binafsi aliwahi kushawishiwa kutia saini kupitisha moja ya miradi iliyoko chini ya wizara yake kwa kuahidiwa kupatiwa dola za Marekani 200,000 (Sh. milioni 320), lakini hakushawishika na baadaye kuamua kuufuta mradi huo.
Alisema yapo matukio ya wizi wa nyaya na mafuta ya transfoma, lakini wezi ni Watanzania na wanaokaa gizani baada ya wizi ni Watanzania wenyewe.
Alisema hakuna yeyote ambaye yuko tayari kuwataja wezi wanaokwamisha miradi mbalimbali yenye manufaa kwa taifa, na badala yake watu wamebaki kulalamika.
Alisema katika utekelezaji wa miradi, wizara itamwezesha mwekezaji, ambaye yuko tayari kuwekeza kwa manufaa ya serikali lakini si kwa wababaishaji na wezi.
“Hatutaki wababaishaji ambao wanatembea na mikataba ya makubaliano (MOU) mifukoni na kufanya ujanja ujanja, mtu unamfahamu kabisa kula yake tabu halafu anakuja ofisini anataka kuwekeza,” alisema.
Katika kongamano hilo, wadau walipata fursa ya kutembelaa maonyesho ya miradi 29 itakayotekelezwa na kupata maelezo mbalimbali kuhusiana na miradi hiyo.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru