Wednesday 3 July 2013

Mapambano ya polisi, majambazi yaua mmoja



NA LILIAN JOEL ARUSHA
POLISI jijini hapa wamepambana kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi yaliyokuwa yamejificha ndani ya nyumba na kufanikiwa kumuua mmoja.
Jambazi liliouawa, limetambuliwa kwa jina la Lembris Taiko (35), maarufu kama Dk. Mbushi.
Anadaiwa kusakwa kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na kuhusika na matukio mbalimbali ya ujambazi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema Polisi walipambana na majambazi hayo jana saa 11.15 alfajiri katika mtaa wa Onjaftan, Sokoni one.
Alisema Polisi walipata taarifa toka kwa raia mwema kuwa jambazi hilo na wenzake wawili walikuwa ndani ya nyumba moja inayomilikiwa na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Swalehe, ambaye wakati wa tukio hilo hakuwepo.
Kufuatia taarifa hizo, Polisi waliizingira nyumba hiyo na baadhi waliingia ndani na kuwataka waliokuwemo kujisalimisha, lakini  ghafla walianza kushambuliwa na majambazi hayo.
Mapambano ya risasi baina ya polisi na majambazi hayo yalidumu kwa dakika kadhaa, ambapo wawili walifanikiwa kutoroka na Dk. Mbushi aliuawa.
“Huyu Dk. Mbushi tulikuwa tunamsaka kwa muda mrefu sasa, ana matukio mengi ya uhalifu na mauaji hapa Arusha na katika Mikoa ya Dar es Salaam, na Kilimanjaro,” alisema Kamanda huyo.
Alisema baada ya tukio hilo, Polisi walifanya upekuzi katika nyumba hiyo na kukuta bastola aina ya Bereta iliyofutwa namba ikiwa na risasi moja chemba, ganda moja la risasi na risasi tatu za Shotgun na funguo za milango 26.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru