Monday 8 July 2013

Kodi kampuni za simu Serikali kutoa tamko


Na Hamis Shimye
SERIKALI imesema kesho itatoa tamko kuhusu mkanganyiko uliopo juu ya malipo ya tozo ya kila kadi ya simu na kodi inayopaswa kulipwa na kampuni za simu.
Hivi sasa kuna mkanganyiko kuhusu nani anayestahili kulipa tozo hiyo kwa huduma ya mawasiliano kati ya wateja na kampuni za simu.

Umoja wa Kampuni za Simu za Mikononi Tanzania (moat), kwa mara kadhaa umetoa taarifa kwa umma kwamba, ongezeko la kodi kwa kampuni hizo utakuwa mzigo kwa mwananchi.
Kampuni hizo zinatakiwa kulipa kodi ya asilimia 14.5 badala ya asilimia 12.5 ya awali.
Kutokana na nyongeza hiyo ya kodi, moat ilisema itapandisha gharama kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, baada ya kuanza mwaka mpya wa fedha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa upande wake, ilitoa ufafanuzi kuhusu tozo ya sh. 1,000 kwa kila kadi ya simu, ikisema zinapaswa kulipwa na wateja wanaotumia huduma ya mawasiliano.
Akizungumza kwa simu jana, mjini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alisema kesho serikali itatoa tamko kuhusu suala hilo.
Janet alisema kwa sasa serikali haiwezi kusema chochote kwa kuwa yatakuwa majibizano, hususan kutokana na kila mmoja kusema lake kuhusu suala hilo.
“Tutatoa tamko tarehe 10, tutakutana na TCRA na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kueleza kwa kina suala hili pamoja na mchanganuo wote,’’ alisema.
Alisema tamko hilo ndilo litakuwa msimamo wa serikali na litatoa majawabu ya maswali yanayojitokeza, hivyo kuondoa mkanganyiko uliopo.
Naibu waziri alisema anashangazwa na maoni kuwa kodi hiyo itakuwa mzigo kwa mwananchi, kwani kampuni za simu hazisemi ukweli kuhusu suala zima la kodi.
“Kampuni za simu si wa kweli, kwa kuwa hawalipi kodi na pale tunapochukua uamuzi wanasema ni mzigo kwa mwananchi wakati wanafaidika sana,’’ alisema.
Alisema zinawatoza kodi nyingi wananchi katika huduma, lakini hazijawahi kusema ni mzigo kwa wananchi.
Naibu waziri alisema mkutano huo utatoa msimamo wa serikali, baada ya kukutana na pande zote.

WACHUMI WATOFAUTIANA

Kwa upande wao, wataalamu wa uchumi wametofautiana kuhusu tozo ya sh. 1,000 kwa kila kadi ya simu inayotumika.
Walisema uamuzi huo unaweza ukawa na faida kwa nchi na wakati huo huo, ni mzigo kwa mwananchi wa kipato cha chini.
Mhadhiri katika Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Godius Kahyarara, alisema suala hilo ni pana na halihitaji kukurupuka kulijadili.
“Kila kitu lazima kimefanyiwa utafiti kabla hakijaanzishwa, hususan katika masuala ya kodi, hivyo ukilitazama kwa umakini unaweza ukasema ni sahihi wananchi kulipishwa,’’ alisema.
Dk. Kahyarara alisema huu si wakati wa kusema fulani ni kipato cha chini na hawezi kushiriki katika suala la maendeleo.
“Uamuzi wa kuweka sh. 1,000 nahisi utakuwa umefikiwa baada ya kufanyika utafiti wa kina, lakini kiasi hicho si kikubwa ijapokuwa kinapaswa kiangaliwe upya,’’ alisema.
Alisema matatizo yanayoanza kujitokeza, hususan malalamiko yanatokana na mfumo wa kodi kuwa si mzuri.
Naye Dk. Jehovaness Aikaeli, kutoka idara hiyo, alisema tozo hiyo itamtesa mwananchi kwa kumlipisha kodi mara mbili.
“Kampuni za simu zinalipa kodi serikalini, ambapo kodi hizo hutokana na fedha anazokatwa mwananchi katika huduma ya simu, hivyo unapomtaka tena alipe kodi ni kumkandamiza,’’ alisema.
Alisema kama uamuzi wa serikali ni kuongeza kiasi cha kodi, njia hiyo imekwenda kinyume kutokana na kumkandamiza mwananchi kwa kumlipisha kodi mara mbili.
Hata hivyo, Dk. Aikaeli alisema kodi ni suala la muhimu na wananchi wanapaswa kulipa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru