Tuesday 9 July 2013

Mwanafunzi aunganishwa kesi yakina Che Mundugwao


NA FURAHA OMARY
MWANAFUNZI Ahsan Ali Iqbal au Ali Patel (19), raia wa Uingereza, ameunganishwa na washitakiwa wenzake katika kesi ya kula njama na wizi wa vitabu 26 vya hati za kusafiria mali ya serikali.
Iqbal, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa mara ya kwanza Ijumaa iliyopita, akikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya wizi wa hati hizo za kusafiria, kughushi na kuwasilisha hati ya kughushi.
Mshitakiwa huyo, jana aliunganishwa katika kesi inayowakabili mwanamuziki Chingwele Che Mundugwao, Ofisa Ugavi wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kiluwasha, Injinia Keneth Pius wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na mfanyabiashara Ally Jabir.
Mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, alidai hati ya mashitaka imebadilika kwa kuongezwa mshitakiwa Iqbal na kuomba kuwasomea upya mashitaka.
Kweka alidai shitaka la kwanza, linawakabili washitakiwa wote ambalo ni la kula njama ya kutenda kosa.
Alidai Che Mundugwao, Pius, Jabir na Iqbal, katika tarehe tofauti kati ya Aprili 16 na Mei 10, 2013, eneo la Kurasini, waliiba hati za kusafiria 26 zenye thamani ya sh. milioni 1.3, mali ya serikali.
Shitaka la pili, linalomkabili Kiluwasha anadaiwa akiwa mtumishi wa umma, kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu, akiwa katika ofisi za makao makuu ya Idara ya Uhamiaji, Kurasini, aliiba hati za kusafiria 26 zenye thamani ya sh. milioni 1.3, mali ya serikali.
Katika shitaka la tatu linalomkabili Che Mundugwao, Pius, Jabir na Iqbal, wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho, waliiba hati hizo za kusafiria.
Che Mundugwao anadaiwa kuwa Mei 30, mwaka huu, eneo la Yombo Makangarawe, kinyume cha sheria alikutwa na hati 12 za watu wengine.
Pia, anadaiwa siku hiyo alikutwa akimiliki hati mbili za kusafiria halali zilizotolewa  kwa jina lake.
Che Mundugwao na Pius, wanadaiwa Aprili 22, mwaka huu, sehemu isiyofahamika mjini Dar es Salaam, walighushi hati ya kusafiria namba AB 651929, kuonyesha kwamba ni halali na imetolewa na Idara ya Uhamiaji.
Shitaka la saba linamkabili Jabir, ambapo anadaiwa kuwa Aprili 24, mwaka huu, sehemu isiyofahamika mjini Dar es Salaam, alighushi hati ya kusafiria namba AB 651966 kuonyesha imetolewa halali na Idara ya Uhamiaji.
Shitaka la nane, linamkabili Kiluwasha ambaye anadaiwa kuwa, tarehe isiyofahamika mwaka 2007 na 2011, mjini Dar es Salaam, alighushi nyaraka za serikali ambayo ni muhuli, akijaribu kuonyesha kuwa ni halali na umetolewa na Idara ya Zimamoto na Uokoaji
Iqbal anadaiwa tarehe tofauti mjini Dar es Salaam, alighushi hati ya kusafiria yenye namba AB 651926 kuonyesha ni halali na imetolewa na Idara ya Uhamiaji ya Tanzania huku akijua si kweli.
Mwanafunzi huyo anadaiwa Julai Mosi, mwaka huu, katika mpaka wa Kasumulu uliopo Kyela, mkoani Mbeya, aliwasilisha hati hiyo ya kughushi kwa ofisa uhamiaji Koplo Amosi Kilugo, huku akijua ni ya kughushi.
Washitakiwa walikana mashitaka, Wakili Kweka alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.
Hakimu Sundi aliahirisha shauri hilo hadi Julai 22, mwaka huu, kwa kutajwa.
Iqbal na wenzake walirudishwa rumande kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuzuia dhamana yao.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru