Wednesday 10 July 2013

URA kumpa Kibadeni 'First Eleven'


NA MWANDISHI WETU
KOCHA Mkuu wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni, amesema anasubiri kwa hamu mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya URA ya Uganda.
Simba na URA zinatarajia kumenyana vikali katika mchezo huo uliopangwa kuchezwa Julai 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kibadeni, alisema kuwa mchezo huo ni kipimo kikubwa chake kwa kujua kiwango cha kila mchezaji baada ya kufanya mazoezi ya muda mrefu.
Alisema URA ni timu ngumu, hivyo ana matumaini makubwa ya kuanza kutengeneza kikosi cha kwanza 'First
Eleven' kupitia mchezo huo aliodai ni muhimu kwake.
"Huu ni mchezo muhimu sana kwetu, ni mechi ambayo itanipa taswira ya kujua kikosi changu kitakuwaje msimu ujao," alisema Kibadeni.
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, alisema anatarajia kuanika kikosi chake cha wachezaji wapya na zamani na amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi.
Baadhi ya wachezaji wapya waliotua Simba Assumani Kayinzi, Kon James, Ammis Tambwe, Samuel Ssenkoom, Felix Cuipoi, Zahor Pazi, na Issa Rashid 'Baba Ubaya'.
Simba imeanza kuonyesha makali yake katika mechi za kirafiki baada ya kuifumua timu iliyopanda daraja ya Rhino Rangers ya Tabora mabao 3-0.
Kibadeni amejiunga na Simba kurithi mikoba ya Mfaransa, Patrick Liewig, ambaye klabu hiyo ilisitisha mkataba wake baada ya kumalizika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru