Friday, 27 June 2014

Ada elekezi sasa kupangwa vyuoni



SERIKALI imeanza kufanya utafiti wa kina kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kupanga ada elekezi kwa programu zote zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini.


Jenister Mhagama - Naibu Waziri, Elimu na Ufundi
Imesema mwongozo wa ada elekezi ulizinduliwa rasmi Machi 13, mwaka huu, na kwamba ada mpya zitaanza kutumika baada ya utaratibu wa mfumo huo mpya kukamilika.



Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, alipokuwa akijibu swali la Ismail Rage (Tabora Mjini-CCM), aliyetaka kujua gharama za ada za masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vingine nchini.



Jenister alisema kwa sasa Tanzania inavyo jumla ya Vyuo Vikuu 53 na taasisi 21 zinazotoa shahada.



Alisema sera ya elimu ya juu ya mwaka 1999 kifungu cha 6.4.3 kinaruhusu taasisi za elimu ya juu kupanga na kusimamia vyanzo vya mapato, ikiwa ni pamoja na kutoza ada za masomo.



Naibu Waziri alisema gharama za ada ya masomo katika vyuo vikuu hutegemea chuo na programu ambayo mwanafunzi anasomea.



Akitoa mfano wa ada za kozi, Jenister alisema katika programu za uhandisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza sh. milioni 1.3 kwa mwaka wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. milioni 1.5.



Alisema katika programu za sayansi na elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza sh. milioni 1.3 wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. milioni 1.2.



Aidha, alisema katika programu za elimu kwa masomo ya sayansi ya jamii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinatoza ada ya sh. milioni moja wakati Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoza sh. 800,000.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru