NA RACHEL KYALA
WANANCHI mbalimbali jijini Dar es Salaam wametoa maoni yao kuhusu bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015, iliyosomwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya.
Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, wananchi hao wameeleza kufurahishwa na bajeti hiyo, hususan katika masuala ya benki kutakiwa kupunguza riba na kufutwa kwa ushuru katika uhaulishaji wa pesa.
Baadhi ya wananchi wamesema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali kufuta misamaha ya kodi na pia kuongeza ushuru katika bidhaa za pombe na sigara kwa vile ni vitu visivyo na umuhimu katika maisha ya binadamu.
Eric Ollotu, mfanyabiashara na mkazi wa Kariakoo, alisema amefurahishwa na kauli ya Waziri Saada kwamba atafuatilia kuona kwa nini wamiliki wa benki hawajatii agizo la serikali la kushusha riba ili kuwapa unafuu wananchi kukopa kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Alisema riba zinazotozwa sasa na baadhi ya benki ni kubwa na zinawafanya wananchi wengi washindwe kukopa kwa hofu ya kukatwa pesa nyingi na kwa muda mrefu.
Ollotu amelezea umuhimu wa nia ya serikali kutoa ushuru wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti na kutunza kumbukumbu (EFD) kwa mwaka mmoja ili ziweze kupatikana kwa bei nafuu na kupunguza kiwango cha kodi.
Amesema kutolewa kwa ushuru katika mashine hizo, kutasaidia kuhamasisha matumizi yake kwa wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine hizo hivi sasa.
Wakala wa mitandao ya simu, Emmanuel Masinga, alisema amefurahishwa na uamuzi wa serikali wa kufuta ushuru wa 0.15 katika uhaulishaji wa pesa (Money Transfer), badala yake tozo itabaki kwa fedha anazolipa mteja.
Alisema kufutwa kwa tozo hiyo kutawahamasisha wananchi wengi kutumia huduma hiyo na hivyo wao kupata faida zaidi.
Wananchi wengine wameielezea bajeti hiyo kuwa itasaidia kupunguza mfumuko wa bei na hivyo kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.
Wamesema mfumuko wa bei ndio chanzo kikubwa cha watanzania kuwa na maisha magumu, hivyo serikali ilipaswa kulipa tatizo hilo kipaumbele katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha iliyosomwa jana.
Philip Bukuku, mkazi wa Ilala, alisema anaamini bajeti hii itawanufaisha wananchi, kwani wizara nyingi zinazoigusa jamii moja kwa moja, zimepewa kipaumbele kwa maana hiyo zitakuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi.
Amesema ili kupunguza tatizo la mfumuko wa bei, serikali ilipaswa kutoa kipaumbele kwenye Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ili iwe na uwezo wa kuwahudumia wananchi katika kuinua kilimo na hatimaye kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza bei za mazao.
Japhar Mghamba, mkazi wa Buguruni, alisema bajeti imejibu maswali mengi ya Watanzania yaliyokosa majibu kwa kipindi kirefu, kwa kuwa kodi ya petroli itakuwa katika hali nzuri, tofauti na ilivyokuwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha iliyopita.
Pia alisema uamuzi wa serikali kuondoa tozo kwenye matrekta, utasaidia wawekezaji wakubwa kuzalisha bidhaa kwa bei nafuu, hivyo bei ya ujumla ya bidhaa sokoni itaweza kuhimiliwa na wananchi wa hadhi zote.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kusikitishwa kwao kutokana na kupandishwa kwa bei ya vinywaji, hususan vinywaji baridi kwa madai kuwa ni hitaji la muhimu ikilinganishwa na vilevi pamoja na sigara.
Thursday, 12 June 2014
Wananchi wafurahia riba za mikopo benki kupunguzwa
09:09
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru