Na Rashid Zahor, Dodoma
MBUNGE wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia kumuhamisha mara moja Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe.
Mtemvu amesema katika kipindi kifupi alichokaa katika Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi huyo amesababisha matatizo makubwa kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuendesha mambo kibabe.
“Nakuomba mama yangu Hawa Ghasia, tunakuheshimu sana, mkurugenzi wa jiji (la Dar es Salaam) hafai, tuondolee huyu mtu aletwe mwingine,” alisema Mtemvu bungeni juzi alipokuwa akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.“Watu wamekuwa wakionewa bila sababu, Dar es Salaam inaendeshwa kibabe, sisi watu wa pwani hatujazoea kusema na ukiona tunasema, ujue kuna tatizo,”aliongeza.
Kauli hiyo ya Mtemvu iliungwa mkono na Mbunge wa Nyamagana (Chadena), Ezekieh Wenje, ambaye alisema walilazimika kumng’oa mkurugenzi huyo alipokuwa Mwanza kwa njia ya kura.
“Sisi tulimuondoa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kwa kutumia saini za wananchi, tukampelekea Waziri Mkuu. Nawashauri wananchi wa Dar es Salaam nao wafanye hivyo. Sidhani kama wanahitaji mtu wa aina hii,”alisema Wenje alipokuwa akichangia bajeti hiyo.Mbunge huyo aliitaka serikali iwe na mipango ya muda mrefu ya kushughulikia matatizo ya wafanyabiashara wadogo (wamachinga) ili kumaliza migongano ya mara kwa mara kati yao na halmashauri za miji.
Alisema wamachinga wamekuwa wakiongezeka kila siku kutokana na kukosekana ajira kwa vijana, hivyo wanapaswa kuandaliwa mipango mahususi na ya muda mrefu ili waweze kufanya biashara zao bila bughudha na kwa kufuata sheria na utaratibu.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan, aliitaka serikali kuharakisha kuhamishia makao makuu ya serikali mkoani Dodoma kutokana na Jiji la Dar es Salaam kufurika na kutapika.
Alisema kuliacha Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwa makao makuu ya serikali ni kuliweka katika hali mbaya zaidi kwa sababu watu wamejaa pomoni, maghorofa yanakaribia Ikulu na foleni za magari zinatia kichefuchefu.
“Mheshimiwa Spika, naiomba serikali iharakishe kuhamia Dodoma na jambo hili lifanyike kwa haraka kwa sababu Dar es Salaam kumejaa,”alisema mbunge huyo.
“Hivi sasa watu wamejenga maghorofa yanakaribia Ikulu, wanamchungulia Rais Ikulu. Wenzetu kama Nigeria walishahamishia mji wao mkubwa kiserikali Abuja kutoka Lagos, sisi tunasubiri nini?” alihoji mbunge huyo.Alisema foleni za magari katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa zinatia kiichefuchefu kutokana na wingi wa magari na kwamba, watu wamekuwa wakichelewa kazini na kushindwa kufanyakazi kwa ufanisi.
Azzan alisema hata kama mtu atatoka nyumbani kwake saa 11 alfajiri ili awahi kazini, anaweza akajikuta akifika huko saa tatu au saa nne asubuhi.
Kutokana na kauli hiyo ya Azzan, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliamua kumuongezea muda wa dakika mbili mbunge huyo ili aendelee kuchangia bajeti hiyo ya serikali.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru