WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Dk. Titus Kamani, amesema viwanda vyote vinavyotengeneza nyavu haramu
zinazotumika katika shughuli za uvuvi vitachukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Kamani amesema hatua hizo pia
zitachukuliwa kwa wafanyabiashara wanaouza nyavu hizo na wale wanaozinunua na
kuzitumia katika uvuvi kwa vile kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la
Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini-CCM), aliyetaka kujua kwa nini serikali inashindwa
kuwachukulia hatua wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza nyavu hizo na
wanaoziuza kwa vile wanafahamika.
"Wanaotengeneza, wanaoziuza, wanaozinunua na kuzitumia katika uvuvi, wote wanafanya makosa kisheria na watashughulikiwa," alisema.
Akijibu swali la msingi la mbunge
huyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Ole Telele,
alisema serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha wavuvi wadogo kwa
kuhakikisha kuwa zana na vyombo vya uvuvi vinapatikana kwa bei nafuu.
Alisema katika jitihada hizo,
serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika,
nyuzi za kushonea nyavu za uvuvi na vifungashio.
Telele alisema pia kuwa injini za
uvuvi, malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake,
hupewa punguzo la kodi ama kufutiwa kodi kabisa ili kuwawezesha wavuvi kumudu
bei za vifaa hivyo.
Naibu Waziri alisema katika mwaka wa
fedha 2013/2014, Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), kupitia Dirisha la Kilimo,
imewezesha miradi minne ya uvuvi yenye thamani ya sh. bilioni 1.5 katika
halmashauri za Sumbawanga, Ukerewe, Ilemela na Muleba.
Alisema miradi hiyo imewezesha
upatikanaji wa boti nne za uvuvi na vifaa vya kuhifadhia samaki katika Halmashauri
ya Wilaya ya Sumbawanga, boti sita za uvuvi Ukerewe, boti 28 za uvuvi, injini
za boti 20 na boti moja ya doria Ilemela.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru