Monday, 16 June 2014

Mjadala mkali kutikisa bunge


NA SELINA WILSON, DODOMA
MJADALA mkali unatarajiwa kutikisa Bunge leo, wakati wabunge watakapoanza kuchangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2014/2015 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita.
Bajeti hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum,  na kufuatiliwa kwa karibu na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi huku baadhi yao wakipata fursa ya kuwepo bungeni ilipowasilishwa.
Hoja zinazotarajiwa kuteka mjadala huo ni pamoja na kodi ya Payee wanayokatwa wafanyakazi ambayo imepunguzwa kwa kiwango kidogo cha asilimia moja kutoka asilimia 13 hadi 12 tofauti na matarajio yao.
Eneo lingine linalotarajia kuzua mjadala ni ushuru wa asilimia 25 wa magari yanayoingizwa nchini, ambapo kwa sasa kiwango kwa mujibu wa bajeti hiyo kiwango cha muda wa matumizi umepumnguzwa kutoa miaka 10 na zaidi hadi miaka minane na zaidi.
Waziri wa Fedha, Saada aliposoma eneo hilo wakati wa kuwasilisha bajeti wiki iliyopita aliibua gumzo kwa baadhi ya wabunge ambao walionekana kushtushwa huku wengine wakiguna.
Hatua hiyo ilisababisha Spika Anne Makinda, kuingilia kati na kumtaka waziri asubiri kidogo ambapo aliwaulizwa wabunge: “Mnapiga kelele, mmezoea mitumba eeh,” alisema kabla ya kumruhusu aendelee kuwasilisha.
Misamaha ya kodi na serikali kuendelea kutegemea mapato kutoa vinywaji vikali, baridi na sigara  ni mambo ambayo yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa miongoni mwa wabunge watakaopata nafasi ya kuchangia.
Hatua hiyo inatokana na maoni ya baadhi ya wabunge waliyoyatoa muda mfupi baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, wengi wakisema bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Anne, wabunge watapata fursa ya kujadili na kuchangia bajeti kwa siku tano kuanzia leo kabla ya kuipitisha.
Spika Anne alisema kwa utaratibu wa mbunge mmoja kuchangia kwa dakika saba, anatarajia kutoa nafasi kwa wabunge wengi zaidi ili waweze kuchangia kwa upana wake.
“Kwa utaratibu wa dakika saba kwa kila mchangiaji naamini wabunge wengi mtapata fursa ya kuchangia kwa hiyo ambao hawajaomba mkajiandikishe ofisini ili mpate nafasi,”alisema Spika.
Alisema mjadala huo utaanza baada ya kipindi cha maswali na majibu na kwamba wabunge watachangia kwa siku tano mfululizo kabla ya kuingia kwenye hatua nyingine ya kuipitisha.
Wakichangia mjadala huo, wabunge walikuwa na maoni tofauti wakati wengine wakipongeza wengine walisema kwamba hakuna kilichobadilika hivyo wanatarajia mambo kama iliyovyokuwa kwa mwaka huu wa fedha unaomalizika Juni 30.
Hata hivyo tayari serikali, imekubali kuongeza sh. bilioni 200 baada ya Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, kutaka fedha hizo ziongezwe katika bajeti ya miradi ya maendeleo.
Akizungumzia hilo wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema fedha hizo zitapatikana baada ya kukata kwenye mambo yasiyo ya lazima, ikiwemo ununuzi wa magari, kalenda, chai, matamasha, semina na mengine yasiyo muhimu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru