Tuesday, 3 June 2014

Wataalamu wa Cuba kuchuguza Dengue


NA SELINA WILSON, DODOMA
SERIKALI kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Cuba, imeanza kufanya utafiti kuhusu ukubwa wa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa dengue kwa binadamu.
Hatua hiyo inatokana na wagonjwa 1,039 kuthibitishwa  kuwa na virusi vya ugonjwa wa dengue kati ya Januari na Mei mwaka huu, ambao ulilipuka katika jiji la Dar es Salaam.
Katika wagonjwa hao, wamo 10 walioripotiwa katika mikoa na idadi yao kwenye mabano Mbeya (2), Kigoma (3), Kilimanjaro (1), Njombe (1) na Dodoma (1).
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015.
Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Cuba.
Dk. Rashid alisema katika kukabiliana na ugonjwa huo, serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo mabasi zaidi ya 600 yaendayo mikoani kupuliziwa dawa.
Alisema pia wizara imenunua  vipimo 5,700 nchini na mafunzo yametolewa kwa watoa huduma ili kuwapa uwezo wa  kuwabaini wagonjwa wa dengue wanaohudhuria katika vituo vya huduma za afya.
Waziri alisema mpaka sasa hakuna dawa maalumu wala chanjo ya ugonjwa huo bali mgonjwa hutibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huo kama homa na kupungukiwa maji na damu.
Alisema ili kujikinga na ugonjwa huo, wananchi wanapaswa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama kwenye maeneo wanayoishi na waondoe vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vifuu vya nazi, makopo na magurudumu ya magari.
Akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani, Msemaji wa wizara hiyo, Dk Antony Mbassa, alisema wizara inapaswa kuhakikisha taka zote zinateketezwa kwa kufuata kanuni za afya bora na rafiki kwa mazingira.
Dk. Mbassa alisema hatua hiyo itasaidia kuzuia ulipukaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na athari zinazoweza kutokea iwapo taka hizo zitatumiwa ama kuokotwa na watoto kwa matumizi mengine na kudhuru afya zao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru