Na Chibura Makorongo, Shinyanga
SERIKALI imeombwa kulipatia
ufumbuzi tatizo la vijana wanaojiita “wabeshi” wanaovamia mgodi wa almasi wa
Williamson Diamonds Ltd ulioko Mwadui, Kishapu mkoani hapa.
Vijana hao wamekuwa wakivamia
mgodi huo kwa lengo la kupora mchanga wa almasi na kujikuta wakipoteza maisha
au kupata vilema vya maisha.
Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni na wakazi wa vijiji
vinavyozunguka mgodi wa Almasi wa Mwadui ambapo walisema kwa kipindi kirefu
vijana wengi wanaovamia mgodi huo wanapoteza
maisha .
Wakazi hao walisema imefika
wakati sasa kwa serikali kufanya utafiti ili kuweza kuwabaini watu
wanaowafadhili vijana hao kwa kuwapatia fedha kidogo na vitendea kwa kazi kwa
ajili kufanya uvamizi kwa makubaliano ya kuwauzia almasi watakazozipata.
Mkazi wa kijiji cha Masagala,
Hubi Mlyandengu, aliiomba serikali iwachunguze baadhi ya polisi ambao
wanatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa makundi ya wabeshi na kuruhusu vijana hao
kuingia mgodini kwa lengo la kupora mchanga wenye madini ya almasi.
Alisema vijana hao ni sawa bomu
linalosubiri kulipuka kwani kuna hatari kutokea mapigano makubwa kati yao na
walinzi wa mgodi, alitoa mfano wa tukio la wiki iliyopita kundi la wabeshi
likiwa na silaha za jadi lilipovamia mgodini na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Hata hivyo, habari za kuaminika
tayari serikali imeanza mikakati ya kuwadhibiti vijana hao na watu wanaowatuma
na kwamba, operesheni hiyo imekuwa ikifanyika kimya kimya ili kuhakikisha wengi
zaidi wanatiwa mbaroni.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru