SUBIRA SAID NA EVA MBESELE, TSJ
MWANAMKE Amina Maige, mkazi wa
Dar es Salaam, anayedaiwa kumfanyia ukatili msichana wake wa kazi, kwa
kumng'ata meno sehemu mbalimbali na kumsababishia majeraha amekana mahakamani
kutenda kitendo hicho.
Amina alikana kumfanyia hivyo,
Yusta Kashinde, jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, mbele ya Hakimu
Yohana Yongolo, wakati akisomewa maelezo ya awali.
Akimsomea maelezo hayo, Wakili wa
Serikali, Tumaini Mfikwa, alidai Amina (42), mkazi wa Mwananyamala, wilayani
Kinondoni, anafahamiana na Yusta ambaye alikuwa mfanyakazi wake wa ndani.
Tumaini alidai Yusta alianza
kufanya kazi za ndani kwa Amina kuanzia Januari, 2012 hadi Juni 3, 2014.
Alidai mshitakiwa huyo katika
kipindi chote, alikuwa akimng'ata Yusta kwa meno na kumsababishia majeraha.
Wakili huyo, alidai mshitakiwa
alikamatwa Machi 4, mwaka huu na
kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kupandishwa kizimbani Juni
12, mwaka huu.
Baada ya kumsomea maelezo hayo
mshitakiwa huyo ambaye yupo rumande tangu alipopandishwa kizimbani kwa mara ya
kwanza kutokana na upande wa Jamhuri kupinga dhamana, alikubali jina lake,
umri, mahali anapoishi na kwamba anamfahamu Yusta.
Mshitakiwa aliomba mahakama
impatie dhamana kwa kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Hata hivyo, Hakimu Yongolo
alikataa ombi hilo na kumtaka mshitakiwa kuwasiliana na uongozi wa Magereza ili
aweze kupatiwa matibabu.
Hakimu aliahirisha shauri hilo
hadi Julai 10, mwaka huu, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa
upande wa Jamhuri.
Umati wa watu ulifurika
mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia shauri hilo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru