NA JESSICA KILEO
UMOJA wa Vyuo Vikuu nchini, umemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kupuuza watu wanaobeza makadirio ya wizara yake kwa mwaka 2014/2015 aliyowasilisha Bungeni hivi karibuni.
Mwakilishi wa umoja huo kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, Massoro Kivuga, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Kivuga alisema wamejifunza mambo mengi kutoka kwa waziri huyo shujaa na jasiri, ambaye anaweza kufanya mambo makubwa katika nchi.
Alisema wanaombeza wana nia ya kumpotosha ili aonekane hajafanya kitu kupitia Chama tawala na kwamba wanaofanya hivyo, wanajitafutia umaarufu kwa kusimamia dhana ya uongo ambao Profesa Tibaijuka amekuwa akiupinga katika shughuli zake.
Kivuga alisema baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) wanadai hawajaona mambo mazuri aliyofanya Profesa Tibaijuka.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, wao wakiwa kama wasomi wanaona kuwa baadhi ya wabunge wanaeneza uongo ambao si mustakabali wa nchi, na kwamba kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa viongozi shupavu kama alivyo Profesa Tibaijuka.
Pia, alisema Profesa Tibaijuka amefanya mambo mengi mazuri, ikiwemo kusuluhisha migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ikileta matatizo.
“Cha kusikitisha leo hii Halima Mdee anathubutu kusimama na kusema kuwa hakuna mafanikio yaliyopatikana, sisi tulidhani angekuwa wa kwanza kumsifia kutokana na ukweli kwamba juhudi zake zinaonekana,”alisema.
Kwa upande wake, Halima Hamad kutoka Chuo kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kama umoja wa Mataifa wamempongeza kwa kazi zake, hawaoni kwanini viongozi wengine wa ndani kama Halima hawaoni mazuri aliyofanya.
Alisema hizo ni chuki ambazo hazijengi bali zinabomoa na ni wazi kabisa hawamtakii mema kutokana na kung’ang’ania mabaya na kuacha kusema mazuri.
Naye Magambo Kate kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), alisema mti uzaao matunda ndio upigwao mawe hivyo katika utendaji wake mzuri hakosi wapinzani.
Tuesday, 3 June 2014
Wasomi vyuo vikuu wamfagilia Profesa Tibaijuka
08:06
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru