Thursday 12 June 2014

Mwanza yageuka uwanja wa vita


Na waandishi wetu, mwanza na dodoma
KATIKATI ya Jiji la Mwanza jana paligeuka uwanja wa mapambano kati ya wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga), Mgambo wa Jiji na askari polisi huku mabomu zaidi ya 120 yakirindima kwa takriban saa nne na kulifanya eneo hilo lisikalike.
Mabomu hayo yalirindima maeneo mbalimbali ya mji, ikiwemo eneo maarufu la Makoroboi kutokana na kuvunjwa kwa vibanda vya machinga jana asubuhi, hali iliyowafanya wacharuke na kuanza mapambano na askari polisi na mgambo wa jiji huku wakishinikiza wenzao walio kwenye maeneo halali nao waondolewe ili wote waikose Makoroboi.
Wakati hayo yakitokea mkoani humo, serikali ilitoa kauli jana Bungeni mjini Dodoma na kusema suala za operesheni ya kuwaondoa machinga katika eneo la Makoroboi lililosababisha vurugu, linafanyiwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa, baada ya mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Ezekia Wenje, kuomba mwongozo wa Spika kuhusu operesheni hiyo ambayo mara kadhaa imesababisha vurugu jijini Mwanza.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitaka serikali itoe maelezo kuhusiana na suala hilo, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema suala hilo linafanyiwa kazi na majibu yatatolewa.
Katika sekeseke hilo lililoanzia saa 3.58 asubuhi hadi 8.45 mchana, wamachinga zaidi ya 40 wamekamatwa kwa tuhuma za kukiuka sheria za mipango miji.
Hatua hiyo ya kuwaondoa  wamachinga hao katika eneo hilo,inatokana na uamuzi wa Baraza la Halmashauri la Jiji la Mwanza, wa kusafisha biashara ‘chafu’ ya wamachinga kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria.
Imeelezwa kuwa eneo la kutoka barabara ya Lumumba linaloingia Makoroboi hadi kupitia msikiti wa Hindu kwenye shule Rajendra na kuingia barabara ya Nyerere, linatakiwa kuwa wazi. Tukio hilo ni la zaidi ya mara mbili  kutokea kwa wamachinga  kulikalia kwa nguvu.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania, lilitoa askari wake wa kijeshi ‘MP’ kuimarisha ulinzi kwenye vitengo vya mabenki, ofisi za serikali na maeneo nyeti ili kutokwaza shughuli za kila siku kuendelea.
Ofisa wa Zimamoto, Sajenti Meja, Gadafi Masoud, alisema msikiti wa Hindu wanaosali Singa singa umenusurika kuchomwa moto na machinga hao baada ya magari makubwa mawili ya kikosi chake kuuzima moto uliowashwa kwa lengo la kuuteketeza.
Mirindimo hiyo iliyoanza asubuhi hadi mchana, ilisababisha kufungwa kwa maduka katika mitaa mingi ya mjini kati na hivyo kuwapa usumbufu mkubwa wateja kutoka katika mikoa ya jirani ya Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita waliohitaji bidhaa katika maduka ya jumla.
Pia, wakazi na wateja kutoka katika wilaya nne za mkoa wa Mwanza yaani Ukerwe , Magu, Kwimba, Sengerema na Misungwi, walikwazwa katika shughuli zao za kibiashara rejareja na jumla.
Mbali ya mirindimo ya mabomu ili kudhibiti vyema vurugu hizo ambazo zinachochewa na fukuto la kisiasa, polisi mkoani Mwanza waliongeza nguvu ya askari  kutoka wilaya za Magu, Kwimba, Misungwi na Sengerema.     
Usafiri wa daladala kutoka nje ya mji, maeneo ya uwanja wa ndege, Pasiansi, Igoma, Nyakato, Igogo na Buhongwa, uliendelea bila wasiwasi chini ya ulinzi wa polisi huku kipande cha barabara ya Nyerere kutoka kwenye mataa hadi Msikiti wa Ijumaa kikiwa kimefungwa kudhibiti harakati za wamachinga na ‘timbwilitimbwili’ zake za kawaida.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola, hakuweza kupatikana kutokana na kusafiri kikazi. 
Hata hivyo, alipotafutwa msaidizi wake, Christopher Fuime, ilidaiwa yupo katika operesheni hiyo huku baadhi ya askari ambao hawakutaka  kutajwa majina yao, wakisema zaidi ya wamachinga 40 wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
Wakati huo huo, serikali ilitoa kauli yake mjini Dodoma, kutokana na vurugu hizo. 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitaka serikali itoe maelezo kuhusiana na suala hilo, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema suala hilo linafanyiwa kazi na majibu yatatolewa.
“Mheshimiwa Spika, suala hilo limeshaanza kufanyiwa kazi, Waziri Mkuu alikuwa anafanya mawasiliano na viongozi wa Mwanza, amerudi kupiga kura tu, lakini bado anaendelea kulifanyia kazi,” alisema Lukuvi.
Awali, Lukuvi alisema serikali inaandaa na inakusudia kutoa taarifa bungeni kuhusu operesheni hizo za kuwaondoa machinga.
 Hata hivyo, Spika alimkatiza  na kumtaka atoe taarifa kwa ajili ya Mwanza tu kwa kuwa ndicho kilichoulizwa na Wenje.
Katika mwongozo huo, kwa mujibu wa kifungu cha 47(1), Spika alimpa dakika tano Wenje ili aeleze kilichotokea, ambapo alisema Jiji la Mwanza limechafuka kutokana na operesheni ya kuwaondoa machinga eneo la Makoroboi.
Alisema kuna vurugu kubwa zilizosababisha wafanyabiashara kufunga maduka na hivyo kusababisha serikali kupoteza mapato yatokanayo na kodi kutoka kwa wafanyabishara.
Wenje alisema kwa kuwa kumekuwa na vurugu kama hizo, Mwanza, Arusha, Mbeya,Dar es Salaam na Iringa, alitaka serikali itoe kauli bungeni kusitisha operesheni hiyo kwa kuwa inadhuru maisha ya watu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru