Monday, 30 June 2014

UOZA UWANJA WA NDEGE


Dk. Mwakyembe kulipua mtandao hatari wa vigogo

  • Ni baada ya kukabidhiwa  picha za CCTV
  •  Kuonyesha wanavyoshiriki michezo michafu

NA BAKARI MNKONDO
AGIZO lililotolewa na Waziri wa Uchukizi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu taarifa za uhalifu unaofanywa na baadhi ya watumishi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JKIA), zimekamilika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama uwanjani hapo wamekamilisha jukumu lao na kukabidhi taarifa husika kwa Dk. Mwakyembe.
Taarifa hizo zinahusisha picha zilizopigwa na kamera za siri (CCTV) ambazo hutumika kurekodi matukio yanayofanywa na baadhi ya vigogo katika utendaji wao wa kila siku.
Habari zilisema katika baadhi ya picha hizo wataonekana baadhi ya vigogo hao wakiwasumbua abiria kwa kuwatisha na wengine wakipokea mlungula au kutoa lugha chafu.
Hata hivyo, licha ya kupata uhakika wa kukabidhiwa kwa picha hizo, halikufanikiwa kupata majina ya vigogo waliorekodiwa wakijihusisha na vitendo vilivyo kinyume na maadili.
Kuwekwa hadharani kwa picha hizo, kunatokana na agizo lililotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Dk. Mwakyembe alipofanya ziara uwanjani hapo, kuwapongeza masofisa wa ulinzi na usalama.
Maofisa hao walifanikisha kukamatwa kwa raia wa Oman akiwa na dawa za kulevya na kutaka kuwahonga maofisa hao sh. milioni 20 na gari ili wamwachie.
Dk. Mwakyembe alisema anachukizwa na kuwepo kwa watumishi wasiokuwa na uadilifu ambao wamekuwa wakisumbua wageni pindi wanapowasili kwa kujivika majukumuambayo sio yao.
“Nafahamu kila kitu kinachoendelea. Nakuagizeni nipeni taarifa za picha zote zinazowaonyesha watumishi wakichukua rushwa na kuiba marashi ya wageni wakati wa ukaguzi na picha zao nitaziweka katika vyombo vya habari,” alikaririwa akisema
Aliongeza kuwa kuna maofisa wanaofanya ukaguzi wa kuangalia chanjo kwa wageni wanaowasili nchini au kuondoka na ambao wamekuwa wakichukua rushwa kwa raai hao huku wakijipa majukumu ya kuangalia hati za kusafiria.
Dk. Mwakyembe alisema hawezi kuvumilia kuona nchi ikiharibiwa sifa yake na watumishi wanaoendekeza rushwa na kusumbua wateja kutoka mataifa mbalimbali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru