Thursday, 12 June 2014

Majambazi yakufuru



  • Yateka kituo cha polisi, yaua askari
  • Yapora SMG 2, Shortgan 5, risasi 70
  • Chagonja: Tumetuma kikosi kuyasaka

NA RABIA BAKARI
WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi, wakiwa na silaha, wamevamia Kituo cha Polisi Mkamba wilayani Mkuranga na kuua askari mmoja kisha kupora silaha mbalimbali.
Tukio hilo ambalo limewashitua wananchi na hata wanausalama, lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia jana, ambapo mbali na kuuawa kwa askari Kolpo Joseph Ngonyani, pia mgambo wawili walijeruhiwa na hali zao si nzuri.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema majambazi hayo yalivamia kituoni hapo na kumpiga risasi Koplo Ngonyani.
Hata hivyo, alisema Koplo Ngonyani aliikwepa risasi hiyo na kwenda kumpata mgambo Venance Francis sehemu ya begani. Francis alikuwa akisaidia kulinda kituoni hapo.
Kamishna Chagonja alisema baada ya Koplo Ngonyani kukwepa risasi hiyo, majambazi hayo yalianza kumshambulia kwa kumkatakata kwa panga.
Alisema baada ya kutenda unyama huo, majambazi hayo yalipora silaha zilizokuwa kituoni hapo, ambazo ni SMG mbili, ambazo kila moja ilikuwa na magazine yenye risasi 30.
Pia, yalipora bunduki zingine tano, zikiwemo Shortgan tatu zilizokuwa zikisubiri kuchukuliwa kwenda kuhifadhiwa kwenye ghala la kituo kikubwa.
Kamishna Chagonja alisema Koplo Ngonyani alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Kwa upande wake, Francis na mgambo mwingine  Mariam Mkamba, bado wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limetuma kikosi maalumu kilichokwenda kuweka kambi wilayani Mkuranga kwa ajili ya kuendesha msako dhidi ya majambazi hayo.
“Tumeweka kambi kwa ajili ya kufanya msako, ni lazima majambazi haya yakamatwe. Tunaomba wananchi wasiwe na hofu kuhusu usalama wao na watoe ushirikiano kwa polisi pindi wanapokuwa na shaka na mtu,” alisema.
Mapema jana asubuhi, wananchi waliokuwa wakiingia na kutoka wilayani humo walikuwa wakipekuliwa na askari waliokuwa doria kwenye maeneo mbalimbali.
Barabara za kuingia na kutoka zilikuwa zimedhibitiwa na askari, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha majambazi hayo yanatiwa mbaroni.
Kamishna Chagonja amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa majambazi hayo, ambapo aliweka hadharani namba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu ambayo ni 0754 785 557 na 0715 009 953 ambayo ni ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru