Thursday 12 June 2014

Mgambo aliyejeruhiwa na majambazi afariki


NA RABIA BAKARI
MGAMBO Venance Francis, aliyejeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, ambao waliteka kituo cha polisi, kuua askari na kupora silaha, amefariki.
Marehemu  huyo, ambaye alijeruhiwa kwa risasi begani, alifariki jana  wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Tukio hilo la aina yake lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kituo cha Polisi cha Mkamba, kilichoko Kimanzichana, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
Kamishna wa Upelelezi na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema jana kuwa, mgambo mwingine, Mariam Mkamba ambaye ni mmoja wa majeruhi katika tukio hilo, bado anaendelea na matibabu.
Katika tukio hilo, majambazi hayo yalidaiwa kumlenga risasi Koplo Joseph Ngonya, aliyekuwa kituoni hapo, ambapo aliikwepa na kwenda kumpiga marehemu Francis begani.
Baada ya Koplo huyo kukwepa risasi, ndipo walipoamua kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili, na alifariki wakati akipelekwa hospitali kupata matibabu.
Majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbalimbali, zikiwemo SMG mbili  za Jeshi la Polisi, ambazo zilikuwa  na magazine moja moja zenye risasi 30 kila moja, bunduki za kiraia aina ya Shotgun tatu na silaha nyingine, ambazo zilikuwa zikisubiri kupelekwa kituo kikubwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kwenye ghala.
Kamishna Chagonja alisema hadi  sasa  hakuna mtu aliyekamatwa wala kuhusishwa na tukio hilo.
Kwa sasa, Chagonja yupo Mkuranga tangu juzi, akiongoza kikosi kazi cha upelelezi na kwamba bado wanaendelea na taratibu za mazishi kwa  marehemu wote wa tukio hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru