Tuesday 10 June 2014

Kikwete ayaonya mashirika binafsi


NA FURAHA OMARY
RAIS Jakaya Kikwete ameyaonya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOS), kuacha tabia ya kueleza habari mbaya ili yaweze kupatiwa fedha.
Alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi, linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na matumizi ya tovuti, ambayo itakuwa imebeba taarifa mbalimbali za sensa hiyo.
ìNatoa wito kwa wananchi na wadau kusoma na kuzitumia vizuri takwimu hizi, kwa kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa watu kubeza jitihada zilizofanywa na serikali.
ìHata wale wanaojua, wamekuwa wakiudhika  wanaposikia pato la taifa limekuwa, basi wao wanataka habari mbaya tu. Habari mbaya zimekuwa zikisaidia NGOS kupata fedha. Hii siyo njia sahihi ya kupata fedha, kuna mmoja aliwahi kwenda kusema tunalazimisha watu kwenda shule,î alisema.
ìTaarifa hii inaweka wazi ukweli ulivyo.  Zitumieni.  Kama upotoshaji ulikuwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa rejea ya takwimu sahihi, takwimu ndizo hizo kwa kila mmoja wetu kuziona na kuzitumia.  Asiyefanya hivyo ana lake jambo,î alisisitiza.
Alisema kwa mujibu wa chapisho hilo, nchi imepiga hatua kiasi kikubwa ya kuelekea Tanzania tunayoitamani, ambapo alitoa wito kwa watumiaji wengine wa takwimu hizo, zikiwemo idara za serikali, kuhakikisha wanazitumia vizuri kwa ajili ya mipango ya nchi na kusukuma maendeleo ya taifa.
Alisema ili kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020 kwa upande wa Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, tunapaswa kujitazama tulipotoka na tulipo leo, ambapo kwa mujibu wa chapisho hilo, nchi imepiga hatua kiasi kikubwa katika kufikia Tanzania ninayoitamani. 
UMRI WA WATU KUISHI
ìIfikapo mwaka 2016, kutakuwa na Watanzania milioni 50 na mwaka 2025, tutakuwa milioni 63.3 ambao ndio mwaka wa Dira ya Maendeleo. Kwa upande wa Zanzibar, ifikapo mwaka 2020,  kutakuwa na watu milioni 1.8,îalisema.
Rais Kikwete alisema bila ya kufanya hivyo, nchi itarudi nyuma badala ya kwenda mbele kutokana na yale yaliyopangwa, yanakuwa hayaendi sawa.
Kuhusu wastani wa miaka ya kuishi, Rais Kikwete alisema imepanda, ambapo kabla ya Uhuru, ulikuwa miaka 35 kutokana na maradhi mbalimbali, lakini umeongezeka kutoka miaka 50 ya mwaka 1988 hadi kufikia miaka 61 mwaka 2012.
ìTukiwa na umri wa miaka 61, wenzetu duniani ni miaka 70, hivyo tujipe lengo la kufikia miaka hiyo,î alisema na kuongeza kwamba mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali katika kupambana na maradhi.
Awali, akimkaribisha Rais, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema machapisho hayo yatakuwepo mengine 11.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru