Thursday, 12 June 2014

Waliopora NMB wahukumiwa kifo


NA WILLIUM PAUL, MOSHI
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, imewahukumu raia wawili wa Kenya, kunyongwa hadi kufa baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia askari Polisi, wakati wa tukio la uporaji la Benki ya NMB, Mwanga.
Wakati Wakenya hao Samwel Saitoti na Michael Kimani, wakipewa adhabu hiyo, Mtanzania Calist Kanje alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuwa mshiriki mkuu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kakusulo Sambo, alisema baada ya kusikiliza na kutafakari ushahidi uliowasilishwa na mashahidi 18 wa upande wa Jamhuri, mahakama imeridhika kuwa upande wa Jamhuri umethibitisha mashitaka dhidi yao pasi kuacha shaka yoyote.
“Kutokana na ushahidi wa mashahidi wa kwanza, watatu na wa 11, mahakama imeridhika kuwa Saitoti na Kimani ambao ni raia wa Kenya, walimuua kwa makusudi Konstebo wa Polisi, Michael Milanzi kwa kumpiga risasi, hivyo inawaoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa,” alisema.
Jaji huyo, alisema washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa na lengo la kutekeleza ujambazi katika benki hiyo, waliamua Michael kitendo ambacho kisheria adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa. 
Pia, alisema baada ya kutafakari kwa kina maelezo ya Jamhuri pamoja na ya mashahidi wa 8, 16 na 17, mahakama imeridhishwa kuwa mshitakiwa huyo, raia wa Tanzania, alikuwa ni mshirika mkuu wa washtakiwa hao.
Alisema kutokana na ushiriki wake huo, mahakama hiyo inamhukumu mshitakiwa huyo kifungo cha miaka mitano kwa kosa la kuhifadhi na kutorosha watuhumiwa wa mauaji ya askari Polisi huku akifahamu kuwa ni kosa kisheria.
Aidha, mahakama iliamuru fedha ambazo walikutwa nazo washitakiwa hao ambao ni Dola za Marekani 8145 na fedha za Tanzania sh. milioni 1.7 zikabidhiwe kwa benki ya NMB, Mwanga.
Wasitakiwa hao wote walikuwa wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia ya polisi huyo, ambapo ilidaiwa wakiwa na wenzao wengine 9, walishiriki katika tukio la uporaji na mauaji yaliyotokea Julai 11, mwaka 2007 katika Benki ya NMB tawi la Mwanga, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro. 
Raia hao wa Kenya, tayari wanatumikia kifungo kingine cha miaka 67 jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama na kupora sh.million 239 katika tukio la wizi kwenye benki hiyo.
Saitoti na Kimani walitiwa hatiani kwa kosa hilo na kufungwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja huku Mtanzania mwingine Elizabeth Msanze au “Bella”, akihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru