NA MOHAMMED ISSA, MERERANI
ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, imeleta mafanikio na matumaini mapya kwa wananchi na kuipaisha CCM.
Kinana ambaye alifanya ziara katika mikoa ya Tabora, Singida na Manyara, ameongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2010-2015.
Akizungumza jana mjini hapa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema ziara ya Kinana ilikuwa ya mafanikio makubwa na kwamba ameacha neema kila sehemu alizopita.
Nape alisema Kinana amerudisha matumaini kwa wananchi wakiwemo wakulima wa tumbaku mkoani Tabora, ambao walikuwa hawajalipwa fedha zao.
Alisema baada ya wakulima hao kueleza matatizo yao, Kinana alifuatilia na hivi sasa watendaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, wamehamia mkoani Tabora kumaliza matatizo ya wakulima.
Alisema katika mkoa huo, huduma za afya zilikuwa zimezorota na kwamba baada ya ziara ya Kinana, kasi ya kuboresha huduma za afya imeongezeka.
Nape alisema kabla ya ziara hiyo, miradi mbalimbali ya afya ilikuwa imesimama na hivi sasa imeanza kutekelezwa kwa haraka.
Alisema watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wako mkoani humo kufuatilia hali hiyo.
Nape alisema wakati Kinana akiwa mkoani Tabora, alipata malalamiko ya walimu wapya ambao walikuwa hawajalipwa kwa sababu walikuwa hawajaingizwa kwenye mfumo wa mishahara. Alisema tayari walimu hao wameshaanza kulipwa mishahara yao iliyokwama kwa miezi kadhaa.
Kwa mujibu wa Nape, kuna mafanikio mengi yamepatikana katika ziara ya Kinana katika mkoa wa Singida, ikiwa ni pamoja na kupewa sh. bilioni 6.4 na serikali kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Hospitali ya Rufaa.
Nape alisema katika mkoa huo, kasi ya ujenzi wa maabara katika shule za kata imeongezeka na kwamba thamani ya zao la alizeti imepanda kutokana na viwanda vingi kujengwa.
Alisema mkoa wa Singida umepiga hatua kubwa kwa kujenga viwanda vidogo vya kukamua mafuta ya alizeti.
Nape alisema katika mkoa huo, serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maji na kwamba mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, utaanza hivi karibuni.
Alisema mradi huo utakapokamilika, utawaondolea kero ya maji wananchi wa mkoa huo.
Nape alisema mafanikio mengine yaliyopatikana katika ziara ya Kinana ni pamoja na serikali kuajiri watumishi wa afya katika Hospitali ya Hydom. Alisema Kinana alitembelea hospitali hiyo na kuambiwa watumishi wengi wanaondoka na kwenda kutafuta ajira serikalini.
Nape alisema baada ya Kinana kupokea taarifa hiyo, aliahidi kuifanyia kazi ambapo baada ya siku tatu, serikali iliajiri watumishi wa afya 94 katika hospitali hiyo inayomilikiwa na kanisa.
Alisema mbali na kuajiri watumishi hao, serikali imeiongezea ruzuku hospitali hiyo kutoka sh. milioni 200 na kufikia sh. milioni 320.
Nape alisema Kinana akiwa katika mkoa wa Manyara, alikumbana na migororo ya ardhi, ambayo aliahidi kuipatia ufumbuzi wa kudumu. Alisema Kinana aliwaahidi wananchi kuwa atamshauri Rais Jakaya Kikwete ili aweze kuyapatia dawa ya kudumu migogoro ya ardhi mkoani humo.
Nape alisema katika ziara hiyo, wafugaji walikuwa wakimsubiri kwa hamu Kinana ili kumueleza changamoto zao. Alisema baada ya kukutana na wafugaji na kuahidi kuyapatia ufumbuzi matatizo yao, waliahidi kuendelea kuiunga mkono CCM.
Nape alisema Kinana aliwatangazia neema wachimbaji wadogo wa Mererani hali iliyosababisha vijana kulipuka kwa shangwe baada ya kuguswa na maelezo mazuri ya kiongozi huyo.
Alisema mbali na hilo, Kinana aliwaahidi wachimbaji wadogo wa Igunga mkoani Tabora kupatiwa maeneo ya kuchimba.
Nape alisema kasi ya Kinana imewafanya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA) kuweweseka na kugeuka msiba kwa vyama vya upinzani.
Alisema pia ziara ya Kinana imevuna wanachama wapya 12,460.
Nape alisema Katibu Mkuu huyo, alitembea zaidi ya kilomita 9,620, na kuhutubia mikutano 192, pamoja na kukagua miradi zaidi ya 213 ya maendeleo.
Tuesday, 3 June 2014
Ziara za Kinana zaipaisha CCM
08:08
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru