Tuesday, 3 June 2014

Kortini kwa kuuza meno ya tembo



  •  Ni yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tano

NA FURAHA OMARY
WAFANYABIASHARA wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kusafirisha na kuuza meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tano.

Washitakiwa hao, Salivius Matembo (39) na Manase Philemon (39), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka ya uhujumu uchumi.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, Wakili wa Serikali, Pius Hilla akishirikiana na Mwendesha Mashitaka, Jackson Chidunda, waliwasomea washitakiwa hao mashitaka matatu.
Mashitaka hayo ni kujihusisha na nyara za serikali kwa kusafirisha na kuuza meno ya tembo yenye thamani ya sh. 5,435,865,000, kuendesha makosa ya uhalifu na kutoroka chini ya uangalizi wa polisi.
Hilla alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, mwaka huu, katika mkoa wa Dar es Salaam, washitakiwa  walisafirisha na kuuza nyara za serikali.
Alidai walisafirisha na kuuza vipande 706 vya meno ya tembo, vyenye uzito wa kilo 1,889, mali ya serikali bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Pia, alidai washitakiwa hao katika kipindi hicho kwa makusudi waliendesha na kufanya makosa ya uhalifu ya kukusanya, kusafirisha na kuuza kiasi hicho cha meno ya tembo.
Manase alidaiwa kuwa Mei 21, mwaka huu, akiwa katika Hospitali ya Sinza Palestina, Kinondoni, Dar es Salaam, alitoroka chini ya uangalizi wa Ofisa wa Polisi, Beatus, aliyekuwa akimmlinda kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya nyara za serikali na kuendesha makosa ya uhalifu.
Hakimu Moshi alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Wakili Hilla alidai upelelezi unaendelea na kuomba shauri liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Kesi hiyo itatajwa Juni 17, mwaka huu na washitakiwa walirudishwa rumande.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru