Wednesday, 25 June 2014

Wanafunzi waua jambazi lenye SMG



  •  Yalipora mamilioni na kuua mfanyabiashara
  •  Mengine mawili yanaswa Moshi na silaha kali

NA MARCO KANANI, GEITA
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Nyang’wale mkoani Geita, wamefanikiwa kumuua mtuhumiwa wa ujambazi akiwa na SMG, kwa kumshambulia na mawe.
Mtuhumiwa huyo na mwenzake, wakiwa na silaha ya aina ya SMG, juzi walizua taharuki kubwa baada ya kuvamia maduka mawili na kupora kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana na kisha kumuua mfanyabiashara kwa risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea kwa uhalifu huo na kusema tayari mtuhumiwa mmoja ameuawa na mwingine kutiwa mbaroni.
Alisema baada ya tukio hilo la ujambazi lililotokea katikati ya mji wa Geita, majambazi hayo yalikimbilia njia ya Nyang’wale. Wakati wakikimbia, mmoja aligongwa na gari la polisi na mwingine alikimbilia shuleni.
“Baada ya kukimbilia shuleni, wanafunzi walianza kumzingira na kumshambulia kwa mawe kabla ya polisi kufika na kumkuta akiwa kwenye hali mbaya,” alisema.
Watuhumiwa hao walianza kuvamia kwenye duka la mfanyabiashara wa bia la Blue Coast Investment, linalomilikiwa na Ignas Athanas na kupora fedha kisha kuondoka baada ya kupiga risasi moja hewani, kuwatisha watu.
Baada ya hapo, walivamia katika duka la wakala wa kampuni za simu, ambapo yalipora fedha na kumuuwa kwa risasi mmiliki wa duka hilo Gosbert Kulwa (59), maarufu kwa jina la Warwa. Pia walimpora bastola.
Inadaiwa kuwa majambazi hayo yakiwa na pikipiki aina ya Sun LG yenye namba T460 CVQ, yaliondoka kwa kasi huku yakinusurika kugongwa na basi la Sabuni lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Mganza, wilayani Chato.
Wakati wa tukio hilo, shughuli zilisimama kwa muda katika mji wa Geita,  huku watu wakikimbia ovyo kuokoa maisha yao kabla ya polisi kufika na kuanza kuyafuatilia.
Wakati huo huo, PAUL WILLIAM anaripoti kutoka Moshi kuwa, watuhumiwa wawili wa ujambazi wametiwa mbaroni mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kuhusika katika matukio tofauti, huku wakiwa na silaha aina ya shotgun.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Boaz, alimtaja mtuhumiwa mmojawapo kuwa ni Ibrahimu Machaku (18), ambaye alinaswa akiwa na bunduki moja aina ya shotgun Greener iliyokuwa imetakwa kitako.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda huyo alisema Machaku alikamatwa Jumatatu iliyopita, baada ya polisi  kuanzisha msako mkali.
Alisema katika uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa silaha hiyo aliyokutwa nayo mtuhumiwa ni mali ya Chama cha Msingi cha Ushirika cha Legho-Mulo.
Kamanda Boaz alisema silaha hiyo, iliporwa Juni Mosi, mwaka huu, kutoka kwa walinzi waliokuwa wakilinda ofisi za chama hicho.
Pia alisema walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa mwingine wa ujambazi, Laurent Massawe (44), baada ya kukutwa na bunduki aina ya shotgun yenye mitutu miwili iliyokatwa kitako.
Kamanda Boaz alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumapili iliyopita,  maeneo ya Shanty Town, Manispaa ya Moshi, baada ya kupata taarifa ya tukio la  uhalifu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru