Sunday, 22 June 2014

China kufadhili wanafunzi elimu ya ufundi

NA NTAMBI BUNYAZU
Mjumbe wa Baraza la Ushauri wa Kisiasa la China, Dk. Annie Wu, amesema atatoa ufadhili wa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini humo.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kukuza na kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China.
Dk. Wu amekuja nchini kwa mwaliko wa Rais Jakaya Kikwete, ambapo amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome.
Katika mazungumzo hayo alimwambia kuwa anatimiza ahadi yake aliyotoa awali ya kusaidia kuinua elimu ya ufundi nchini.
Dk. Wu alitoa ahadi ya ufadhili wa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini humo, wakati Profesa Mchome alipofanya ziara ya kikazi mwezi huu nchini China na kukutana na kufanya mazungumzo na vingozi mbalimbali.
Kutokana na ufadhili huo uliotolewa na mjumbe huyo, Profesa Mchome alisema ufadhili huo umekuja wakati muafaka, ambapo serikali inaimarisha elimu ya ufundi ili kuwaandaa vijana kujiajiri wenyewe pindi wanapomaliza masomo yao ya ufundi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru