Na Chibura Makorongo, Shinyanga
WANACHAMA wa CCM na wananchi mkoani Shinyanga wametahadharishwa kutopotoshwa na kauli zinazotolewa na kikundi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanaopendekeza uwepo wa muundo wa serikali tatu.
Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na Katibu wa CCM mkoani Shinyanga, Adam Ngalawa, alipohutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Didia wilayani Shinyanga ambapo aliufananisha UKAWA na ndoa ya mkeka.
Ngalawa alisema UKAWA wamekuwa wakipita sehemu mbalimbali nchini na kuwashawishi Watanzania waunge mkono mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanayopendekeza muundo wa serikali tatu ambao iwapo utakubalika, utasababisha kuvunjika kwa Muungano uliopo.
“Ndugu zangu tahadharini sana na UKAWA wanashabikia muundo wa serikali tatu. Huu muundo haufai, tukiukubali utatuvunjia Muungano wetu ulioasisiwa na viongozi wetu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. UKAWA ni sawa na ndoa ya mkeka, maana walikurupuka katika kuungana kwao.
“Leo hii nataka niwape siri moja, mmoja wa wajumbe wa UKAWA Maalim Seif Shariff Hamad ni miongoni mwa watu waliokuwa wakipinga muundo wa serikali tatu, huyu ndiye aliyetoa siri za aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe kwamba alipanga kuleta muundo wa serikali tatu, leo hii vipi ashabikie muundo huo?.
“Lazima tuelewe iwapo tutaukubali muundo wa serikali tatu, basi huu Muungano tulionao hivi sasa utakufa, maana kila nchi itakuwa inajiendeshea mambo yake yenyewe. Ule mshikamano wa Tanzania kama nchi moja hautakuwepo tena, kwa hali hii tuhakikishe muundo huu tunaukataa,” alisema.Ngalawa alisema CCM ina kila sababu za kupigania muundo wa serikali mbili kwa vile ndiyo pekee wenye uhakika wa kuendeleza na kudumisha Muungano uliopo hivi sasa, ambapo aliwaomba wana CCM na wananchi wengine kwa ujumla kuhakikisha wanapiga kura ya kuikataa rasimu ya katiba, iwapo Bunge litaipitisha ikiwa na muundo wa serikali tatu.
Katika hatua nyingine katibu huyo aliwapongeza wakazi wa kata ya Didia kwa uamuzi wao wa kuamua kujenga Kituo cha Polisi kwa lengo la kukabiliana na matukio ya uharifu na kwamba, CCM kwa upande wake itawaunga mkono katika ujenzi huo.
“Tunakupongezeni kwa juhudi hii mliyoionesha, ujenzi wa kituo hiki utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu yaliyokuwa yakijitokeza katika kata yenu ambapo hivi karibuni mliwapoteza ndugu zetu wawili waliouawa kikatili na majambazi, CCM tutawaunga mkono kwa kuchangia ujenzi huu,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru