NA RABIA BAKARI
MABASI yanayopendekezwa kutumika kwenye usafiri wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam, ni yale yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 150 kwa pamoja.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Watanzania wengi hawana uwezo wa kumudu kununua magari hayo kwa mtu mmoja mmoja, na kwamba kama wana nia ya kuingia katika biashara hiyo, hawana budi kuungana au kushirikiana na wadau wengine wa usafirishaji.
Kauli hiyo ilitolewa na serikali jana, wakati wa mkutano na wadau kutoka nchi mbalimbali duniani ili kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa mradi huo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwaeleza wadau nia ya serikali kuruhusu uwekezaji katika mradi huo ili kuhakikisha huduma bora na endelevu za usafiri jijini Dar es Salaam.
Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alisema wamiliki wa daladala nchini, hawajaonyesha dalili ya kutaka kuungana hivyo kuwa ngumu kwao kuweza kuingia kwenye mradi huo.
Kuhusu mradi huo, Pinda alisema umeanzia mkoani Dar es Salaam kwa sababu ni mji unaokuwa kwa kasi, ambapo licha ya kuwekeza kwenye mradi pia wanaangalia namna nyingine ya kuboresha usafiri, ikiwemo kujenga miundombinu mbalimbali, akitolea mfano wa daraja la Kigamboni.
Alisema mradi huo ambao umepangwa kufanyika kwa awamu sita, ulianzishwa kwa lengo la kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
“Ubora wa barabara hizi unatarajiwa kuwa wa kiwango kitakachodumu kwa takribani muda wa miaka 15 na serikali inaamini kimefikiwa.
“Aidha, mradi hautakuwa njia pekee kutoka katikati ya jiji kwenda nje bali kutakuwa na njia mbadala ambazo ni pamoja na usafiri wa boti kuanzia Kivukoni hadi Mbweni,”aliongeza.
Pinda aliutaja usafiri wa reli aliouanzisha Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kama wa majaribio, umeonekana kukubalika na utaimarishwa, ikiwemo barabara za juu ambazo pia zinatarajiwa kupunguza tatizo la msongamano kwa kiasi kikubwa.
Awali, Sagini alisema lengo la mkutano huo ni kuzungumzia namna ya uendeshaji wa mradi, ukatishaji tiketi na utengenezaji wa mabasi.
Aliongeza kuwa wanafanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika uendeshaji wa mradi, na kwamba mabasi yatakayotumika yamependekezwa kuwa na urefu angalau wa futi 12, yenye uwezo wa kubeba watu 150 kwa pamoja.
“Pia tiketi zitakazotumika, si hizi zilizozoeleka, na ndiyo maana mmesikia tumezungumzia tiketi hadi za kadi za kielektroniki,”alisema.
Aliongeza kuwa kwa kiasi kikubwa ujenzi wa barabara za DART awamu ya kwanza umekamilika, hivyo wanatengeneza vituo zaidi na wataanza na mabasi 20 kwa majaribio.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, aliishukuru Benki ya Dunia (WB), ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mradi huo.
Tuesday, 3 June 2014
Mabasi mradi wa DART kubeba abiria 150
08:06
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru