Thursday, 12 June 2014

Bajeti


Na waandishi wetu
SERIKALI imetangaza Bajeti ya mwaka 2014/2015 ya sh. Trilioni 19, ambayo imejikita zaidi katika kuimarisha usafiri wa reli, usambazaji wa nishati ya umeme vijijini na kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Pia, kama kawaida imetangaza kuongeza ushuru wa vinywaji baridi, ikiwemo soda na pombe kali huku ikiweka sheria kali ya kuzuia uingizaji wa magari chakavu, kutoka miaka kumi hadi minane na zaidi.


Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema serikali imelenga kuboresha mapato, kuimarisha usafiri wa reli na barabara pamoja na elimu bora kwa kujenga madarasa na mabaara. 
Alisema bajeti ya mwaka huu imelenga kuongeza makusanyo ya mapato, hasa ya ndani kwa kuanzisha vyanzo vipya na kuboresha vilivyopo pamoja na kupunguza misamaha ya kodi. 
Pia, kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika, kuboresha elimu, kuunganisha nchi kwa njia ya miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege. 
Saada alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, ikiwemo upatikanaji wa maji, nishati ya uhakika pamoja na upatikanaji wa elimu bora.
Alisema katika kuhakikisha serikali inadhibiti mapato na kusimamia bajeti kwa ufanisi, inakamilisha utaratibu wa kusimamia na kuyalipa madai ya wakandarasi yaliyohakikiwa kupitia Hazina kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika. 
Pia, alionya kuwa kuanzia sasa wizara na taasisi zinapaswa kuzingatia mfumo wa malipo (IFMS), ambao unamtaka kila Ofisa Msuuli kutoingia mikataba bila kuwa na LPO inayotokana na mfumo wa malipo wa IFMS.
Hata hivyo, alionya kuwa ili bajeti hiyo iweze kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa, nidhamu ya hali ya juu inatakiwa kwa watendaji na viongozi wa serikali na taasisi zake pamoja na wabunge na wananchi.

Mgawanyo wa fedha kwa sekta
Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1,090.6 kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). 
Pia, kiasi kingine cha sh. bilioni 151 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam; na sh. bilioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia Gesi wa Kinyerezi I. 
Kwa mujibu wa Saada, hatua hiyo ya serikali inalenga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana ili kupunguza gharama kwa wananchi hivyo kusaidia kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira.
Katika kuhakikisha inaboresha miundombinu na usafirishaji, Saada alisema kiasi cha sh. bilioni 2,109 zimetengwa, ambapo sh. bilioni 179.0 zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa reli ya kati, ambapo ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja umetengewa sh. bilioni 1,414.8.
Hatua hiyo ni mikakati ya kuendelea kupunguza msongamano wa magari mijini, gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa ili kupunguza mfumuko wa bei.
Katika kuhakikisha elimu inaendelea kuboreka zaidi, Saada alisema kiasi cha sh. bilioni 3,465.1 zimetengwa, ambapo sh. bilioni 307.3 zimetengwa kugharamia mikopo ya elimu ya juu.
Aidha serikali itaendelea kuimarisha ubora wa elimu, ikijumuisha miundombinu ya elimu, hatua ambayo itasaidia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kuimarisha na kujenga madarasa na maabara. 
Pia, vijana wameendelea kupewa fursa mbalimbali ili kuondokana na changamoto, ambapo vyuo vya ufundi stadi vitaimarishwa zaidi.

Wafanyakazi kupumua 
Serikali imependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato, ikiwemo kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 13 hadi asilimia 12.
Imesema hatua hiyo inalenga kutoa unafuu wa kodi kwa wafanyakazi.
Saada alisema serikali itaendelea kuangalia uwezekano wa kupunguza kiwango hiki hatua kwa hatua ili kuwapa nafuu wafanyakazi.
Pia, imependekeza kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha ya kutoa misamaha ya kodi kwa miradi inayohusu upanuzi wa ukarabati inayofanywa na wawekezaji.
Waziri huyo wa Fedha, alisema msamaha huo,  hivi sasa unatolewa kwa utaratibu ambapo wawekezaji hupewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji (TIC).
Aidha, imependekeza kuongeza kiwango cha kutozwa kodi kwenye mapato ghafi ya wafanyakazi wadogo yanayozidi sh. 4,000,000 kwa mwaka na yasiyozidi sh.7,500,000 kwa mwaka; kutoka asilimia mbili hadi asilimia nne kwa mauzo, kwa wanaoweka kumbukumbu za mauzo na kuongeza kutoka sh. 100,000 hadi sh. 200,000 kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizi za kodi ya mapato zitaongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh. milioni 31,504.

Bodaboda, magari  chakavu kitanzini
SERIKALI imetangaza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili na Uhamishaji wa Magari Sura ya 124 ili kutofautisha mfumo wa usajili wa magari na pikipiki.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti uhalifu unaofanyika kwa kubadilisha namba za magari na kuweka kwenye pikipiki kwa lengo la kukwepa kodi.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema hayo bungeni jana, wakati akiwasisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015, ambapo alisema kwa sasa pikipiki zitakuwa na namba zinazoanzia TZ badala ya T. 
Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza mapato ya serikali yanayokwenda mifukoni mwa wajanja.
Pia, alisema serikali itabadili ukomo wa umri wa magari yasiyo ya uzalishaji, yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilimia 25 kwa sasa kutoka miaka kumi na zaidi hadi miaka minane na zaidi. Hatua hiyo inatajwa kuwa itasaidia kulinda mazingira na kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu, ambayo yamekuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani.
Alisema watanzania wamekuwa wakipoteza maisha kwa ajali za barabarani, ambapo pamoja na mambo mengine, uchakavu wa magari umekuwa chanzo.
“Ajali nyingi za barabarani zinasababishwa na uchakavu wa magari, hatua hii itasaidia pia kupunguza gharama za kuagiza vipuri mara kwa mara,” alisema Saada.
Pia, alisema ukomo wa umri wa magari ya uzalishaji na yasiyobeba abiria yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilima tano kwa sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka minane na zaidi. 

Viwanda vya saruji kulindwa
WAZIRI wa Fedha, Saada Salum Mkuya, amependekeza kuondoa saruji katika orodha ya bidhaa zinazofikiriwa kuwa za mtaji, ambazo hupata msamaha wa kodi hivi sasa kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC). 
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuhamasisha uzalishaji wa saruji hapa nchini na kulinda viwanda vya saruji kutokana na ushindani wa saruji inayoagizwa nje.
Saada aliyasema hayo jana bungeni, mjini Dodoma, ambapo pia alipendekeza kufuta misamaha ya kodi iliyokuwa inatolewa kwa kampuni za simu  pale wanapoingiza nchini au kununua bidhaa za mtaji.
“Misamaha hii ni ile inayotolewa kwenye vifaa kama; minara ya mawasiliano, jenereta, uzio wa minara, magari, vifaa vya kujikinga na radi na kadhalika,” alisema.
Pia, alipendekeza kupunguza kiwango cha Ushuru wa Mauzo ya Nje unaotozwa kwenye ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 90 au sh. 900 kwa kilo moja hadi asilimia 60 au sh. 600 kwa kilo moja kutegemea kiwango  kipi ni kikubwa.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuzuia biashara ya magendo ya ngozi ghafi. 
“Uchambuzi unaonyesha kuwa hivi sasa hakuna ngozi ghafi zinazosafirishwa nje kupitia vituo vya forodha na badala yake hupelekwa nje ya nchi kwa magendo,” alisema.
Alisema lengo ni kuongeza usindikaji wa ngozi hapa nchini ili kuongeza thamani na ajira, ambalo bado halijafanikiwa.
Hata hivyo, alisema hatua hiyo, inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh. milioni 5,778.7

Bia, sigara bei juu
SERIKALI imependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, ambapo bidhaa zisizokuwa za mafuta zitatozwa ushuru wa bidhaa kwa asilimia 10. 
Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, aliyasema hayo jana alipokuwa akiwasilisha bungeni mjini Dodoma, mapendekezo ya serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka 2014/2015.
Alizitaja  bidhaa hizo kuwa ni vinywaji baridi, mvinyo, pombe na vinywaji vikali.
Saada alipendekeza ushuru wa vinywaji baridi, kutoka sh.91 kwa lita hadi sh. 100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la sh. tisa tu kwa lita huku ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini, kutoka sh. tisa kwa lita hadi sh.10 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la shilingi moja tu kwa lita.
Pia, inapendekezwa ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda, ambayo hayazalishwi hapa nchini kutoka sh. 110 kwa lita hadi sh.121 kwa lita, sawa na ongezeko la sh. 11 kwa lita.
Kwa upande wa ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa , mfano kibuku, kutoka  sh. 578 kwa lita hadi sh.635 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la sh. 34 tu kwa lita na ushuru wa bia nyingine zote kutoka sh. 578 kwa lita hadi sh.635 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la sh. 57 tu kwa lita.
Alisema ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka sh. 160 kwa lita hadi sh. 176 kwa lita, ikiwa ni ogezeko la sh. 16 tu kwa lita.
Saada alisema ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka sh. 1,775 kwa lita hadi sh. 1,953 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la sh. 178 kwa lita.
Alisema ushuru wa vinywaji vikali kutoka sh. 2,631 kwa lita hadi sh. 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la sh. 263 kwa lita.
Saada alisema ushuru wa bidhaa kwenye maji yanayozalishwa viwandani hautaongezeka.
Aidha,  alisema bidhaa za sigara zitatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 25 ili kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku wa Shirika la Afya Duniani.
Marekebisho ya viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara ni kama ifuatavyo:-
Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka sh. 9,031 hadi sh. 11,289 kwa sigara elfu moja. 
“Hii ni sawa na ongezeko la sh. 2,258 kwa sigara elfu moja au sh.2.25 kwa sigara moja,” alisema.
Alisema sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka sh. 21,351 hadi sh. 26,689 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la sh.9.65 kwa sigara moja.
Kwa upande wa sigara nyingine zenye sifa tofauti kutoka sh. 38, 628 hadi sh. 48,285 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni ongezeko la sh. 9,657 sawa na sh. 9.65 kwa sigara moja.
Pia, tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa sigara kutoka sh.19,510 hadi sh.24,388 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la sh. 4,879 kwa kilo na ushuru wa ‘ Cigar’ unabaki kuwa asilimia 30.
Alisema hatua hizo katika ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 124,292.0
Saada alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba huu kwa kuwa unalingana na azma ya serikali ya kulinda afya za wananchi wake. 
Mbali na hilo, serikali inapendekeza kufuta ushuru wa bidhaa wa asilimia 0.15 unaotozwa kwenye uhaulishaji wa fedha  ili kuwapa nafuu watu wanaotuma fedha kwa kutumia benki na kwa kutumia njia za simu. 
Waziri huyo, alisema badala yake, anapendekeza kuweka ushuru wa asilimia 10 kwa benki na mawakala kwenye mapato wanayoyapata kwenye tozo na ada wanazokusanya kwenye shughuli za uhawilishaji wa fedha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru