NA SELINA WILSON, DODOMA
TANZANIA imeendelea kufanya vizuri katika biashara ya nje, ikiwemo huduma za utalii na usafirishaji bidhaa kupitia nchini kwenda nchi jirani na hivyo kuongeza mapato.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2013 na mpango wa maendeleo wa taifa wa 2014/2015.
Wassira alisema kwa mwaka 2013, katika huduma za utalii, mapato yaliongezeka kutoka dola bilioni 1.37 mwaka 2012 hadi kufikia dola bilioni 1.81 mwaka jana.
Alitaja eneo lingine la usafirishaji bidhaa kupitia Tanzania kwenda nchi jirani, ambapo mapato yaliongezeka kutoka dola milioni 497.3 mwaka 2012 na kufikia dola milioni 576.8 kwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa Wassira, mizigo iliyopitishwa nchini kwenda nchi jirani, iliongezeka kutoka tani milioni 1.175 hadi kufikia tani milioni 1.386 katika kipindi hicho.
Akizungumzia kuhusu akiba ya fedha za kigeni , Wassira alisema imeendelea kuimarika katika kipindi kilichoishia Desemba 2013, ambapo akiba ilifikia dola milioni 4.676 ikilinganishwa na dola milioni 4.069 mwaka 2012.
Kuhusu mapato ya kaya, Wassira alisema matokeo ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya kwa Tanzania Bara, yanaonyesha Watanzania wanaoishi chini ya kiwango cha mahitaji ya msingi, kilipungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 na kufikia asilimia 28.2 mwaka juzi.
Katika jiji la Dar es Salaam, alisema idadi ya kaya ilipungua kutoka asilimia 14.1 mwaka 2007 na kufikia asilimia 4.1 mwaka juzi ulipofanywa utafiti huo.
Aidha katika maeneo mengine ya mijini, kiwango hicho kilipungua kutoka asilimia 22.7 hadi asilimia 21.7 kwa kipindi hicho, na matokeo hayo yanaonyesha kwa jumla asilimia 9.7 ya watu wote waishio Tanzania Bara, wapo chini ya mstari wa umasikini wa chakula, ikilinganishwa na asilimia 16.6 kwa kigezo cha 2007.
Akizungumzia mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2014/2015, alisema ni wa nne katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2011/2012-2015/2016) na kwamba unazingatia vipaumbele vya mpango huo.
Alisema vipaumbele vilivyozingatiwa ni kuhakikisha raslimali chache zilizopo zinatumika katika maeneo muhimu, hususani miradi iliyopo chini ya BRN, ambayo ni nishati, miundombinu, kilimo na maji.
Thursday, 12 June 2014
Sekta za utalii, usafirishaji zaongeza mapato
09:08
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru