WATU 12 wameuawa na wengine 137
kujeruhiwa katika matukio tisa ya ulipuaji mabomu yaliyotokea katika mikoa ya
Arusha, Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.
Aidha, watu 25 wamekamatwa katika
tukio la ulipuaji bomu lililofanyika hivi karibuni katika eneo la darajani
kisiwani Zanzibar, ambapo mtu mmoja alifariki. Watano kati ya watu hao,
wameshafikishwa mahakamani.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Ame Silima, alipokuwa akijibu swali la
Waride Bakari Jabu (Kiembesamaki-CCM), aliyetaka kujua kauli ya serikali kuhusu
matukio ya uhalifu wa kutumia tindikali na ulipuaji mabomu yaliyotokea hivi
karibuni.
Silima alisema katika juhudi za
kukabiliana na matumizi haramu ya tindikali, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkemia Mkuu wa Serikali ya
Muungano na ya Zanzibar, liliendesha
operesheni kubwa ili kupunguza matumizi holela ya tindikali. Alisema operesheni
hiyo imeonyesha mafanikio makubwa.
Naibu Waziri alisema kwa sasa Jeshi
la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio yaliyotokea katika mikoa hiyo
sita, ambapo wataalamu wamefanikiwa kubaini aina za mabomu yanayotumika na nchi
yanakoundwa kama silaha za kivita.
"Kwa sasa timu hiyo inaendelea na uchunguzi wa kisayansi ili kubaini waingizaji na walipuaji wa mabomu hayo," alisema.
Silima alisema serikali imejidhatiti
kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa aina zote na hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachothibitika kuhusika na
matukio ya uhalifu wa matumizi ya mabomu na tindikali.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa
mara kwa moja kwa jeshi hilo iwapo watawabaini watu au kikundi chochote
kinachofanya vitendo vinavyoashiria uhalifi, hasa wa mabomu na tindikali.
Akijibu swali la nyongeza la mbunge
huyo, Silima alisema upelelezi wa matukio hayo hauwezi kuwekwa hadharani, hasa
katika hatua za awali kwa vile kufanya hivyo ni kuharibu upelelezi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru